IQNA

Mkaligrafia wa Kiirani atumia Sanaa ya Qur'an kuimarisha Mahusiano ya Kimataifa

21:18 - October 26, 2025
Habari ID: 3481419
IQNA – Mkaligrafia wa Kiirani, Bi Tandis Taghavi, amesema kuwa anatumia sanaa ya kuandika Qur'an Tukufu kama njia ya kuwasilisha mafundisho ya dini na kuimarisha uhusiano wa kitamaduni baina ya mataifa, katika maonesho ya hivi karibuni ya Iran na Korea Kusini.

Bi Taghavi, ambaye ni mtafiti, msanii wa kaligrafia na balozi wa utamaduni na sanaa katika Kituo cha Kuratibu Utamaduni wa Asia, alishiriki katika maonesho ya kaligrafia ya Iran-Korea yaliyofanyika katika makazi ya Balozi Kim Jun-pyo wa Jamhuri ya Korea mjini Tehran wiki hii. Tukio hilo lilikuwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 63 ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.

Akizungumza na IQNA, Bi Taghavi alisema kuwa kupitia sanaa ya kaligrafia aliandika aya za Qur'ani na mafundisho ya dini mbalimbali kwa muktadha wa familia. Maonesho hayo yalifanyika chini ya kaulimbiu ya “Familia”.

Alisisitiza kuwa kaligrafia ni sanaa ya ustaarabu. “Tunaweza kutumia maneno bora kabisa kupitia sanaa ya kaligrafia… Na sanaa hii ni lugha ya mazungumzo ya ustaarabu baina ya mataifa.”

Aliongeza kuwa ni jukumu letu kuhifadhi urithi huu na kuurithisha kwa vizazi vijavyo.

Maonesho hayo yaliwaleta pamoja wasanii wa Kiirani na wa Kikorea wakifanya kazi bega kwa bega, na yaliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Korea mjini Tehran na Kituo cha Kuratibu Utamaduni chini ya Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia (CCCACD), tarehe 23 Oktoba.

Bi Taghavi alieleza kuwa kaulimbiu ya “Familia” ilitumika kama daraja baina ya imani na tamaduni tofauti. Ingawa kuna tofauti za kiimani kati ya Iran na Korea, alisisitiza kuwa mizizi ya ustaarabu wao ina mfanano.

“Katika maonesho haya, kaligrafia ilitumika kama chombo cha amani na urafiki. Iliweka tofauti hizi kando kwa njia ya heshima na staha.”

Alihitimisha kwa kusema, “Matamanio yangu kama askari wa taifa langu ni kwamba kupitia shughuli za kitamaduni, tuzidi kujenga ukaribu na mataifa ya dunia. Diplomasia ya kitamaduni ndiyo msingi wa diplomasia ya kisiasa.”

3495153

captcha