
Kulingana na vyombo vya habari vya Uingereza, wanaume hao wawili walipelekwa mahakamani baada ya vilipuzi kupatikana pande zote mbili za mpaka, kufuatia uchunguzi wa njama iliyodaiwa kuandaliwa na kundi la itikadi kali za mrengo wa kulia dhidi ya msikiti uliopo Galway, pamoja na maeneo yanayowahifadhi wahamiaji.
BBC iliripoti kuwa Garrett Pollock (35) kutoka Annalong, County Down, na Karolis Peckauskas (38) kutoka Drogheda, County Louth, waliwasilishwa katika kikao maalumu cha Mahakama ya Kaunti ya Portlaoise baada ya polisi wa pande zote kugundua vilipuzi wakati wa operesheni ya pamoja ya kupambana na ugaidi.
Pollock alishtakiwa kwa kumiliki vilipuzi katika maeneo mawili: O'Moore Place, Portlaoise na Kilhorne Green, County Down. Polisi wa Ireland (Gardai) walipinga dhamana, wakisema mashtaka ni mazito, kuna hatari ya mtuhumiwa kutoroka, na kwamba wanaamini anaweza kuwa “tishio kwa dola.”
Afisa mpelelezi Declan O’Connor aliieleza mahakama kuwa video ilipatikana kwenye kifaa kilichokamatwa nyumbani kwa Pollock, ikionyesha wanaume wanne wakiwa wamefunika nyuso zao, wakisimama mbele ya bendera ya rangi tatu. Katika video hiyo, walitoa vitisho vya kushambulia “msikiti wa kwanza wa Ireland” uliopo Galway, pamoja na vituo vya makazi ya kimataifa vya wahamiaji na hoteli zinazowahifadhi.
Jaji Andrew Cody alisema video hiyo inaonekana kama “mazoezi ya taarifa ambayo ingetoa baada ya shambulio la kigaidi kufanikiwa.” Aliongeza kuwa wanaume hao walidai kuhusika na “uharibifu wa msikiti wa kwanza nchini Ireland.”
Kwa sababu hiyo, Cody alisema video hiyo inaimarisha mashaka ya polisi kuwa Pollock ni mmoja wa wanaume waliokuwa kwenye video, na akakataa kutoa dhamana. Pollock alipelekwa rumande hadi kufikishwa tena Alhamisi ijayo.
Peckauskas, ambaye pia alishtakiwa kwa umiliki wa vilipuzi, aliambia mahakama: “Sielewi.” Mkalimani aliteuliwa kumsaidia, na yeye pia alipelekwa rumande hadi kusikilizwa wiki ijayo.
Kulingana na kituo cha matangazo cha RTE, polisi pia walipata waraka uliotajwa kama “manifesto” ya kundi hilo wakati wa upekuzi. Inasadikiwa kuwa video hiyo ilirekodiwa Portlaoise, ingawa haikuwa imesambazwa mtandaoni.
3495312