IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

'Mfumo wa Wamagharibi umefeli, mfumo Mpya umejitokeza duniani'

6:52 - September 06, 2014
Habari ID: 1446839
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullahil-Udhmaa Sayyid Ali Khamenei amesema kuwa, mabadiliko yanayojiri hivi sasa yanatokana na kubadilika mfumo uliokuwa umeasisiwa na Wamagharibi wa Ulaya na Marekani, na kujitokeza mfumo mpya.

Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo Alkhamisi mjini Tehran aliponana na wajumbe wa Baraza la Wanachuoni Wataalamu (Linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu) na sambamba na kutoa uchambuzi jumla kuhusu hali ilivyo hivi sasa ulimwenguni na katika eneo la Mashariki ya Kati na hali ya nchini Iran na ishara za kuanza kuundika mfumo mpya katika dunia, amebainisha sababu kuu zilizopelekea kutetereka misingi ya kifikra na kielimu ya ubeberu wa Magharibi na mfumo unaotawala hivi sasa duniani na kusisitiza kwamba: Katika kipindi hiki nyeti, jukumu kuu la taifa la Iran ni kuongeza nguvu na uwezo wake kwa ajili ya kuwa na taathira na sauti katika suala zima la kuundika mfumo mpya duniani na kwamba kuongeza nguvu na uwezo kunatakiwa kusimame juu ya misingi mitatu mikuu nayo ni nguvu za sayansi na teknolojia, nguvu za kiuchumi na nguvu za kiutamaduni.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amekumbusha kuwa: Umoja na mshikamano ni jambo muhimu mno kwa nchi na ni jukumu la watu wote nchini kuiunga mkono serikali na taasisi za utendaji na utumishi wa umma.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Ayatullah Udhma Khamenei amemshukuru na kumsifu Ayatullah Mahdavi Kani, shakhsia maarufu na wenye thamani kubwa, ambaye ndiye mkuu wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu na ambaye hivi sasa amelazwa hospitalini na kumuombea dua ya kupata ahueni ya haraka. Vile vile amewaenzi wajumbe wa baraza hilo ambao wametangulia mbele ya Haki katika miezi ya hivi karibuni na kuwausia watu wote watumie vizuri baraka za Mfunguo Pili (Dhul Qa'ad), ambao ni mwezi wa toba na kurejea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kwa ufafanuzi wa kina hali inayotawala dunia na eneo la Mashariki ya Kati hivi sasa na kusema: Matukio yanayoshuhudiwa duniani hivi sasa yanaonyesha kuwa mfumo wa dunia ambao ulianzishwa miaka 70 iliyopita na Wamagharibi yaani madola ya Ulaya na Marekani hivi sasa unabadilika na mahala pake pameanza kuchukuliwa na mfumo mpya.
Ayatullah Udhma Khamenei baada ya hapo amezungumzia misingi miwili mikuu ya mfumo wa kutawala dunia uliowekwa miaka 70 iliyopita na madola ya Magharibi ambao mosi umesimama juu ya nguvu za kifikra na thamani za Kimagharibi na pili juu ya nguvu za kijeshi na kisiasa. Ameongeza kuwa: Matukio ya hivi karibuni duniani na katika eneo la Mashariki ya Kati yanaonesha kwa uwazi kuwa misingi yote hiyo miwili ya nguvu za Magharibi imekumbwa na msukosuko mkubwa.
Amegusia msingi wa fikra na thamani walizojiwekea Wamagharibi katika mfumo wao na kusema: Kwa miaka mingi Wamagharibi wamekuwa wakitoa madai yaliyojaa hila za kidanganyifu za kuwalaghai watu kama vile kudai kuwa wanapigania uhuru, demokrasia, haki za binadamu na kuwalinda wanadamu ili kuzifanya thamani walizoziainisha katika mfumo wao zitawale katika maeneo mengine duniani na ndani ya dini za mataifa mbali mbali hasa ndani ya dini tukufu ya Kiislamu. Amesema inasikitisha kuona kuwa katika ulimwengu wa Kiislamu kuna baadhi ya shakhsia na baadhi ya tawala za mataifa ya Waislamu zimeathiriwa na madai hayo na zinaamini kuwa thamani zilizomo ndani ya mfumo wa Kimagharibi ni bora kuliko hata matukufu ya dini yao na inasikitisha kuona kuwa fikra hiyo hadi hivi sasa ingali ina wafuasi katika ulimwengu wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhusu msingi wa kisiasa na kijeshi wa mfumo wa Magharibi pamoja na utamaduni wa Kimagharibi kwamba: Kila yaliponyanyukia mataifa, au tawala au mirengo ambayo haikubali kuburuzwa na Magharibi na ikasimama kidete kupambana na mfumo huo wa Kimagharibi, basi Wamagharibi walitumia nguvu zao zote kuweka mashinikizo ya kisiasa na kijeshi na kuna mifano mingi ya vikwazo na mashinikizo hayo katika nchi mbali mbali ikiwemo Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Mfumo wa Magharibi ulitumia vyomo vya kipropaganda ambavyo kila leo vinazidi kupata nguvu na kuwa vya kisasa zaidi kwa ajili ya kupanua wigo wake ulimwenguni kupitia kuitangaza na kuipigia propaganda misingi hiyo miwili mikuu ya mfumo wa Magharibi ndani ya mataifa mengine na kwamba Magharibi ilikuwa inafanya kila iwezalo kubadilisha mitazanmo ya kifikra ya wasomi wa mataifa mengine na kujaribu kuyakinaisha yaamini kuwa thamani za Kimagharibi ndizo thamani bora kabisa duniani.
Vile vile ameashiria namna misingi yote hiyo mwili ya mfumo wa Magharibi ilivyokumbwa na msukosuko mkubwa hivi sasa na kubainisha sababu zilizopelekea mfumo huo kukumbwa na msukosuko huo kuwa ni misingi ya kifikra na kithamani waliyojiwekea Wamagharibi yaani ubeberu wa kimaanawi wa Magharibi. Amesema: Mgogoro wa kimaadili unaozidi kuongezeka huko Magharibi kama vile kupata nguvu na kuenea sana mambo ya kipuuzi na yasiyo na maana, kukosekana usalama wa kisaikolojia hususan kati ya vijana, kutetereka misingi ya kifamilia, kuwa na mtazamo ghalati kuhusu kadhia ya mwanamke na kuwekwa chini ya alama ya kuuliza harakati za kulinda haki za wanawake na kugeuka mambo machafu kuwa vitu vya thamani kama vile ndoa za watu wa jinsia moja na kutothaminiwa harakati za kupambana na vitendo vya vichafu ni sababu ya kwanza kabisa iliyoutumbukiza kwenye misukosuko msingi wa kifikra na kithamani wa mfumo wa Magharibi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuongezeka fikra ya kupenda dini hasa ya Uislamu na kuzingatiwa mafundisho ya Qur'ani kati ya watu wa nchi za Magharibi, kuwa ni sababu ya pili iliyoutumbukiza katika misukosuko mikubwa msingi wa kifikra na kithamani wa mfumo wa Magharibi. Vile vile ameashiria kujitokeza ukinzani na mgongano wa kivitendo baina ya vitendo na na nara na kaulimbiu zinazodaiwa kupiganiwa na Magharibi na kuongeza kuwa: Magharibi ambayo daima inadai kupigania uhuru, haki za binadamu na demokrasia, yenyewe inakanyaga kaulimbiu zake hizo katika vitendo kiasi kwamba leo hii walimwengu wanaona kichefuchefu wanapowasikia Wamagharibi wanatoa madai ya kupigania uhuru, haki za binadamu na demokrasia.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria takwimu za ajabu za namna Magharibi inavyounga mkono mapinduzi ya kijeshi dhidi ya tawala huru zilizochaguliwa kidemokrasia na kuongeza kuwa: Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, baada ya Vita vya Pili vya Dunia, Marekani imeshapindua serikali 50 na kuchukua makumi ya hatua za kupambana na mirengo ya muqawama wa wananchi dhidi ya tawala za vibaraka wake.
Amesema kitendo cha Marekani cha kutumia bomu la atomiki na kuua watu laki mbili huko Japan, kuanzisha kwake jela kama za Guantanamo na Abu Ghuraib na makumi ya jela nyingine za siri huko Ulaya ni mfano mwingine unaoonyesha kuweko mgongano baina ya maneno na matendo ya Wamagharibi. Ameongeza kuwa, kutumia mabavu, machafuko na ukandamizaji ikiwa ni pamoja na vikwazo dhidi ya mataifa na tawala ambazo zinapingana na ubeberu, kufanya mauaji na kuanzisha makundi ya kigaidi na kuyavamia kijeshi mataifa mengine hususan huko Iraq na Afghanistan na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara nchini Pakistan ni sababu ya nne iliyopelekea kukumbwa na msukosuko msingi wa kifikra na kithamani ya mfumo wa Magharibi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja sababu ya tano na ya mwisho iliyopelekea msingi wa kifikra na kithamani wa mfumo wa Magharibi uingie katika msukosuko mkubwa ni kuanzishw kwao makundi kama vile ya al Qaida na Daesh na kuongeza kuwa: Ijapokuwa Wamagharibi na hasa Wamarekani wanadai kuwa hawana uhusiano wowote na makundi hayo, lakini ushahidi mbali mbali unaondoa shaka kabisa ya kwamba madola ya Magharibi na vibaraka wao katika eneo la Mashariki ya Kati hawahusiki na mkundi hayo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Mambo hayo yameutia katika msukukosuko mkubwa mfumo wa kifikra na kithamani uliowekwa na Magharibi licha ya kwamba Wamagharibi wanafanya kila njia kuonyesha kuwa thamani zao ndizo bora zaidi duniani kiasi kwamba leo hii tena madai yanayotolewa na Magharibi ya kupigania haki za binadamu, demokrasia na uhuru hayana thamani hata chembe kwa walimwengu.
Baada ya hapo amezungumzia sababu zilizoutumbukiza kwenye msukosuko mkubwa msingi wa nguvu za kijeshi na kisiasa wa Magharibi akisema kuwa: Jambo kubwa lililozitumbukizwa kwenye changamoto na msukukosuko mkubwa nguvu za kijeshi na kisiasa za Magharibi ni kuasisiwa mfumo wa utawala uliosimama juu ya msingi wa fikra za Kiislamu na harakati ya kimapinduzi nchini Iran nchi ambayo ipo katika moja ya maeneo yaliyokuwa na ushawishi mkubwa wa Magharibi ambapo mfumo huo mpya wa utawala nchini Iran umeweza kusimama kidete kwa miaka mingi na si tu haukufutwa katika uso wa dunia licha ya kukumbwa na mashambulizi ya kila namna ya kisiasa, kijeshi, kiusalama na kiuchumi ya Magharibi lakini pia hivi sasa umekuwa ni mfumo imara na wenye nguvu na ushawishi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu wa nchini Iran ni mfumo wenye nguvu lakini wakati huo huo ni mfumo uliodhulumiwa. Ameongezaa kuwa, kusimama imara taifa la Iran katika vita vya miaka minane vya kujihami kutakatifu (vita vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya utawala mchanga wa Kiislamu wa Iran) si jambo dogo hata chembe kwani kusimama kidete huko kulithibitisha kwamba nguvu za kijeshi na kiusalama za madola ya kibeberu haziwezi kushinda na wala kupunguza kusimama imara taifa fulani.
Ayatullah Udhmna Khamenei vile vile ameyataja matukio ya hivi karibuni katika eneo la Mashariki ya Kati vikiwemo vita vya siku 33 nchini Lebanon, vita vya siku 22 na vya siku nane vya Ghaza na vita vya hivi vya karibuni kabisa vya siku 50 huko Ghaza kuwa na masuala yaliyosababisha kukumbwa na msukosuko mkubwa nguvu za kijeshi na kisiasa za Magharibi.
Amesisitiza kuwa: Vita vya hivi karibuni vya Ghaza ni mfano wa kimuujiza kwani kusimama imara wananchi katika eneo moja dogo na lililozingirwa kila upande kumeupigisha magoti utawala wa Kizayuni ambao ni nembo ya nguvu za Magharibi katika eneo la Mashariki ya Kati na kwamba wananchi wa Ghaza licha ya kung'ang'aniwa sana na utawala wa Kizayuni ukiwataka wakubali kusimamisha vita lakini walikataa kufanya hivyo hadi pale masharti yao yalipokubaliwa.
Vile vile ameashiria mitazamo ya baadhi ya watu wenye ushawishi huko Magharibi kuhusiana na kwamba chaguo la nguvu za kijeshi na machaguo mengine yenye itibari hayako tena kwa manufaa ya Wamagharibi na kuongeza kuwa: Maana ya maneno hayo ni kuwa uwezo wa kijeshi na kiusalama wa Magharibi umekumbwa na msukosuko mkubwa hivi sasa.
Baada ya kubainisha sababu za kukumbwa na msukosuko mkubwa misingi ya nguvu za kibeberu za Magharibi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mambo yote hayo ni dalili zinazothibitisha kuwa, mfumo unaotawala duniani hivi sasa hauwezi kuendelea, bali kuna mfumo mpya umeanza kujiunda lakini swali muhimu hapa ni kuwa, jukumu letu sisi katika kipindi hiki nyeti sana ni lipi?
Ayatullah Udhma Khamenei amejibu swali hilo kwa kukumbushia nukta mbili. Nukta ya kwanza ni mambo yanayojiri ulimwenguni na katika eneo la Mashariki ya Kati na wajibu wa kuyaelewa vizuri na kuchukua tahadhari yasije nchini Iran yakachanganuliwa kwa sura isiyo sahihi na iliyo kinyume kabisa na uhalisia wa mambo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kuna baadhi ya watu katika eneo la Masharibi ya Kati bali hata baadhi ya tawala za eneo hilo yanaamini kuwa katika kukabiliana na Magharibi hatuna njia nyingine isipokuwa moja tu nayo ni kusalimu amri mbele ya ubeberu wa nadola ya Magharibi. Watu na nchi hizo zinaamini kuwa kama zitakubali kusalimu amri na kukubali kuburuzwa na matakwa ya Wamagharibi, basi Wamagharibi hawataziwekea mashinikizo ya kiuchumi na kisiasa na wala hawatatumia nguvu za kijeshi dhidi yao.
Hata hivyo amesema kwa kusisitiza kuwa: Mtazamo huo ni ghalati na ni makosa, bali ni mtazamo hatari sana. Kwani matukio yanayojiri duniani na katika eneo hili yanaonyesha wazi namna misingi ya nguvu za Magharibi inavyosukwasukwa, hivyo kuna wajibu wa watu kuutambua vizuri uhakika wa mambo ili wasije wakakumbwa na madhara ya kutochanganua mambo kwa njia sahihi.
Nukta ya pili ambayo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ni wajibu kuizingatia hivi sasa ni kujiweka tayari na kujiandaa kuwa na nafasi muhimu katika mfumo wa dunia kupitia kuimarisha na kuitia nguvu nchi.
Ayatullah Udhmna Khamenei ametaja mambo ya lazima ya kuiimarisha na kuitia nguvu nchi kuwa ni kutumia uwezo wote wa ndani na nje ya nchi kufanikisha suala hilo. Ameongeza kuwa: Wapenzi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati wanachunguza kwa kina mikakati yetu kama ambavyo katika eneo la Amerika ya Latini pia na katika sehemu muhimu za bara la Asia watu wanaangalia kwa kina mikakati na stratijia zetu, hivyo ni wajibu kuitumia vizuri fursa hiyo.
Amesema kuwa, mambo matatu makuu yanayoiimarisha nchi na kuongeza nguvu za nchi ni mosi sayansi na teknolojia, pili uchumi na tatu ni utamaduni. Ameongeza kuwa: Serikali, viongozi na watumishi wote nchini wanapaswa kuyapa uzito wa hali ya juu mno masuala hayo matatu na wafanye kazi bila ya kuchoka ili kuiandalia nchi mazingira ya kuwa na nguvu zaidi na zaidi katika masuala hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la idadi ya watu na kuongezeka idadi ya vijana kuwa ni moja ya mambo muhimu mno yanayolipa nguvu taifa na kuhusiana na suala la utamaduni amesema: Kati ya mambo yote matatu makuu ya kuipa nguvu na uwezo nchi, suala la utamaduni ndilo muhimu zaidi kwani linafungamana na itikadi na imani za watu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia namna madola ya Magharibi yalivyowekeza mno katika vyombo vyao vya habari ili kuathiri na kuharibu imani na itikadi za watu wa mataifa mengine na kuongeza kuwa: Kuliwekea mikakati mizuri suala hilo ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho ndani yake, kuandaa mipango mizuri ya kubainisha mambo inavyotakiwa na kwa sura ya kukinaisha watu kuhusu imani na itikadi zao - uwanja ambao ni wa maulamaa, watangazaji, taasisi za tablighi na utamaduni pamoja na vyombo vya habari hususa Shirika la Televisheni na Redio la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB - na kuimarisha na kutia nguvu imani za kidini za watu, ni mambo muhimu sana yanayopaswa kufanywa katika uwanja huo.
Kuhusu suala hilo amesema kwa kugogoteza kwamba uhusiano baina ya maulamaa na matabaka mbali mbali ya wananchi ni moja ya mambo yasiyo na mbadala katika kufanikisha suala hilo na kuhusu umuhimu wa umoja na mshikamano hivi sasa amesema: Ijapokuwa katika masuala ya kisiasa kuna tofauti za kimitazamo lakini suala hilo halipaswi kuruhusiwa kuondoa umoja na mshikamano nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia pia ulazima ya kuungwa mkono kikamilifu viongozi nchini na kuongeza kuwa: Kwa baraka na taufiki ya Mwenyezi Mungu, viongozi wote Serikalini, katika Chombo cha Mahakama na taasisi nyinginezo wanafanya jitihada kubwa sana na serikali nayo katika kipindi cha mwaka huu mmoja wa tangu kuingia kwake madarakani imefanya kazi nyingi na kupata mafanikio mengi.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amesisitiza kwa mara nyingine kuwa kazi za utendaji na utumishi serikalini ni nzito sana na kusema kuwa: Kuiunga mkono Serikali na taasisi zote za utendaji ni jukumu la kila mtu nchini.
Ameongeza kuwa: Tab'an jambo hilo halina maana ya kwamba Serikali isikosolewe. Pia inabidi tukumbuke wakati wote kama ambavyo nimesema mara nyingi kwamba upeo wa mustakbali wa nchi yetu uko wazi sana na kwamba mustakbali wa nchi yetu utakuwa bora kuliko nchi zote duniani.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Ayatullah Hashemi Shahroudi, Naibu wa Kwanza wa Mkuu wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria namna mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unavyozidi kuimarika siku baada ya siku na kusema kuwa ushindi wa wanamuqawama wa Kiislamu huko Palestina, Syria, Iraq na Lebanon ni katika baraka za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ameongeza kuwa Imam Khomeini (quddisa sirruh) hakuwa muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu katika nchi moja tu, bali ni chimbuko la mabadiliko adhimu na makubwa katika ulimwengu mzima wa Kiislamu.
Naibu wa Kwanza wa Mkuu wa Baraza la Wanavyuoni Watalaamu ameashiria hatua zilizochukuliwa na maadui za kuleta uharibifu na upotoshaji wa harakati za Kiislamu na ametaka kuwekwe mipangilio madhubuti ya kukabiliana na njama na hila hizo za maadui.
Naye Naibu wa Pili wa Mkuu wa Baraza la Wanachuoni Watalaamu, Ayatullah Yazdi ametoa ripoti kuhusu kikao cha siku mbili kilichofanyika hivi karibuni cha baraza hilo.
Ayatullah Yazdi ametaja baadhi ya mambo muhimu yaliyojadiliwa katika kikao cha hivi karibuni cha Baraza la Wanavyuoni Wataalamu (Linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu) kuwa ni pamoja suala la utamaduni na udharura wa kuzingatiwa zaidi na zaidi masuala ya utamaduni nchini likiwa ni jambo muhimu sana ambalo linaleta ulazima wa kuwekewa siasa na mikakati yake maalumu ya kusimamia na kuendesha muundo wa kijamii, na vile vile kuitaka serikali kuupa uzito wa hali ya juu ustawi wa kiuchumi na udharura wa kuitoa nchi katika hali ya kuzorota na kuhakikisha kuwa siasa za uchumi wa kusimama kidete zinatekelezwa ipasavyo. Amesema hayo ni miongoni mwa masuala makuu yaliyojadiliwa na wajumbe wa baraza hilo katika kikao chao kilichomalizika siku chache zilizopita.

1446624

captcha