IQNA

Kikao cha kwanza cha 'Fikra ya Pamoja kati ya Wanachuo wa Ulimwengu wa Kiislamu'

10:57 - November 27, 2008
Habari ID: 1713213
Kikao cha kwanza cha 'Fikra ya Pamoja kati ya Wanachuo wa Kiislamu' kilianza jana Alkhamisi katika Chuo Kikuu cha Tehran hapa mjini Tehran. Kwa mujibu wa shirika la habari la IQNA, Dawoud Gudarzi, Katibu wa kikao hicho amezungumza katika ufunguzi wa kikao hicho na kubainisha mipango na malengo ya kikao hicho cha siku tatu.
Amesema, kikao hicho kinafanyika chini ya anwani, 'Karne ya 21, Karne ya Kuimarika Uislamu.' Wasomi na wanafikra mashuhuri wa ulimwengu wa Kiislamu akiwemo Hassan Rahimpur Azgadi, mwanafikra na mtafiti mashuhuri wa Kiislamu wameshiriki katika kikao hicho. Mtafiti huyo amezungumza katika kikao hicho kwa kuwasilisha maudhui ya 'kuhuishwa maisha ya Uislamu katika karne ya 21.' Wasomi wengine walioshiriki katika kikao hicho ni pamoja na Abdallah Muhammad Sheikh Idris, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanachuo wa Sudan, Nidhal Ammar, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanachuo Waarabu, Dakta Barakat, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Damascus na Abdallah Hamid Bankala, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanachuo Waislamu wa Nigeria. Zaidi ya wanafikra na wanachuo wa Kiislamu 250 wanashiriki katika kikao hicho cha wanachuo wa Ulimwengu wa Kiislamu. Kikao hicho kinafanyika kwa lengo la kujua uwezo na vipawa vya Ulimwengu wa Kiislamu ili kuwaunganisha Waislamu, kunufaika na fikra za wasomi na wanafikra wa Kiislamu katika kuunufaisha umma wa Kiislamu, mshikamano na umoja katika kutetea maslahi na haki za Waislamu na hasa katika nchi za Iraq, Palestina, Afghanistan na Lebanon na kuimarisha urafiki na udugu miongoni mwa jamii za Kiislamu. Maidhui muhimu zitakazojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na Ulimwengu wa Kiislamu katika mtazamo wa Imam Khomeini (MA), uchunguzi wa hali ya nchi za Kiislamu katika melenea mpya, ubeberu wa Magharibi na jinsi ulivyodhihiri na kushuka, Ulimwengu wa Kiislamu na njama za Magharibi, mpango wa Mashariki ya Kati Kuu na Mpya, Nato ya kiuatamaduni na udiplomasia wa umma (utamaduni na vyombo vya habari) katika mtazamo wa nchi za Magharibi na njama za kutusiwa matukufu na thamani za Kiislamu. 326178
captcha