IQNA

Athari za wanafalsafa wawili wa Kiislamu kwa falsafa ya Magharibi kuchunguzwa nchini Hispania

9:37 - December 02, 2008
Habari ID: 1714857
Kuchunguzwa athari za fikra za kifalsafa za Ibn Sina na Ibn Rushd katika ulimwengu wa Magharibi, ni moja ya malengo ya kufanyika kikao cha Chuo Kikuu cha Complutense cha mjini Madrid, Hispania.
Akizungumza na shirika la IQNA kutoka mjini humo, Ahmad Ridha Khudhari, Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni cha Jamhuriya Kiislamu ya Iran nchini Hispania amesema kuwa moja ya njia za kuhamishwa elimu kutoka nchi za Mashariki na hasa Iran kuelekea Magharibi na fikra za wanafalsafa kama vile Ibn Sina kuelekea ulimwengu wa Magharibi, ilitimia kupitia wasomi na wanafalsafa wa Kiislamu waliokuwa wakiishi Andalusia, yaani Hispania ya leo.
Akibainisha kuwa kikao cha ‘uchunguzi wa fikra za Ibn Sina na Ibn Rushd katika utamaduni wa Kiislamu’ kitafanyika siku ya Alkhamisi ijayo tarahe Nne Disemba, katika chuo kilichotajwa kwa mnasaba wa kutimia milenia moja tokea afariki dunia Ibn Sina, Khudhari ameongeza kuwa, Ibn Rushd aliishi miongo kadhaa baada ya kuaga dunia Ibn Sina lakini aliathirika sana na fikra za tabibu na mwanafalsafa huyo mashuhuri wa Kiislamu. Khudhari ameendelea kusema kuwa, kikao hicho kitafanyika katika hatua tatu ya vikao vya kielimu, meza duara na miziki ya kienyeji ambapo wanafikra na wasomi wa Kiislamu na wasio Waislamu watashiriki na kutoa mchango wao kuhusiana na nafasi ya wanafalsafa hao wawili wa Kiislamu.
Ni muhimu kukumbusha hapa kwamba, fikra na vitabu vya wanafalsafa hawa wawili na hasa vya Ibn Sina vinafundishwa na kutumiwa katika mifumo ya masomo ya vyuo vikuu muhimu vya nchi mbalimbali za Magharibi. 328035
captcha