Katika mahojiano yake maalumu na IQNA balozi wa Umoja wa Visiwa vya Comoro nchini Iran, Ahmad Najid Al Marzuqi ameashiria aya ya 103 ya Sura Al Imran isemayo “Na Shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarakiane” na kusema aya hii inapaswa kuchukuliwa kama kigezo na Waislamu wote ili wasitengane katika njia ya Mwenyezi Mungu. Amesema Waislamu hawapasi kuruhusu wasiokuwa Waislamu kuzusha masuala ya kuwafarakanisha kama vile kutenganisha baina ya Masuni na Mashia. Ameongeza kuwa Waislamu wana chimbuko moja na kwa hivyo iwapo upande mmoja utapata madhara, mwili wote wa umma pia utadhurika. Amesema, Waislamu wa madhehebu ya Shia na Suni wote kwa pamoja wako chini ya bendera ya “La ilaha Illa Allah, Muhammad Rasullullah” yaani “Hakuna mola apasaye kuabudiwa Ila Allah, na Muhammad ni Mtume wake”. Mwanadiplomasia huyo wa Comoro amesema, maadui wa Uislamu wamevamia Palestina, Syria na Iraq na sasa wanazitisha nchi zote za Kiislamu. Amesema, vitisho hivyo vya maadui vinatokana na kukosekana Umoja miongoni mwa Waislamu na kutofuata maamurisho ya Mtume Muhammad SAW kuhusu umoja. Amekumbusha kuwa katika Qura'ni Tukufu Mwenyezi Mungu pia ameashiria udharura wa kuwepo umoja miongoni mwa Waislamu. Amesema, aya isemayo “Hakika Umma huu wenu ni Umma mmoja” inaashiria takwa la Mwenyezi Mungu la kuwepo umoja miongoni mwa Waislamu. Balozi Ahmad Najid Al Marzuqi amekosoa ukosefu wa umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu na kusema: “Baadhi ya nchi za Kiislamu zinaziruhusu nchi za kigeni kuingilia mambo yao ya ndani na kuzusha mifarakano miongoni mwa Waislamu”.
Katika kujibu suali kuhusu mikakati ipi ifanyike kuleta umoja miongoni mwa Waislamu, balozi huyo amesema: “Hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu kuna watu wanaofanya juhudi za kuwakurubisha pamoja Waislamu wote na kuinua hali yao ya maisha. Iran inaongoza katika harakati za kuutetea Uislamu na Waislamu. Hii inatokana na misingi iliyowekwa na hayati Imam Khomeini ambaye katika umri wake wote alijitahidi na kufanikiwa kuanzisha serikali ya Kiislamu na kuwaunganisha Waislamu. Ameongeza kuwa Imam Khomeini alijitahidi katika njia ya mapenzi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wa Uislamu SAW. Amesema, Ayatullah Khamenei ameendeleza mkondo wa thamani wa mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Balozi wa Comoro nchini Iran amesema kuwa: Uzoefu unaonyesha kwamba kufanyika mikutano ya kimataifa kama vile “Kongamano la Umoja wa Kiislamu” ambalo limekuwa likifanyika Tehran kila mwaka pamoja na Mashindano ya Kimataifa ya Quran ambayo pia yamekuwa yakifanyika kila mwaka nchini Iran ni fursa nzuri ambayo huwafanya Waislamu wa mataifa mbalimbali kujuana zaidi. Balozi huyo ameendelea kusema kuwa: "Iran ikilinganishwa na nchi nyingine za Kiislamu kama Saudi Arabia na Misri, iko mstari wa mbele katika kuanzisha uhusiano na nchi za Kiislamu na imechukua hatua nzuri kuzisaidia na kuonyesha mshikamano na nchi za Kiislamu. Lakini ifahamike kuwa hatua hizi hazitoshi katika kukabiliana na njama za maadui za kuzusha mifarakano miongoni mwa Waislamu”.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Ahmad Najid Al Marzuqi ameashiria hali ya mafunzo ya Kiislamu na Qur'ani nchini Comoro. Amesema, utamaduni wa watu wa Comoro umejengeka katika misingi ya Uislamu na kuongeza kuwa kabla ya kuja mkoloni Mfaransa, Kiarabu kama lugha ya Qur'ani, ilikuwa ndio lugha rasmi ya watu wa Comoro. Amesema, pamoja na kuwepo njama za wakoloni za kuuangusha ustaarabu wa Kiislamu, lugha ya Kiarabu imeweza kuhifadhiwa katika utamaduni wa umma.
Balozi wa Comoro mjini Tehran amesema kuwa watoto wote nchini Comoro hupata masomo ya Qur'ani na Uislamu kabla ya kujiunga na shule za Kifaransa. Hata hivyo ameelezea masikitiko yake kuwa hali katika madrassa za Kiislamu ni ya kusikitisha ikilinganishwa na shule za Kifaransa. Amesema kuwa Chuo Kikuu cha Kiarabu na Kiislamu cha Comoro kinatoa mafunzo ya Fiqhi, Hadithi na kadhalika.
Ahmad Najid Al Marzuqi amesema madhehebu ya Kishia yanajulikana kote Comoro na kuongeza kuwa Wacomoro wanawapenda Ahul Bayt AS. Mwanadiplomasia huyo amesema, Wacomoro huandaa mashindano ya Qur'ani kwa minasaba mbalimbali kama vile kuanza mwaka mpya wa Hijria, Eid Fitr na Ghadir, Miladun Nabi SAW na kadhalika.
Ahmad Najid Al Marzuqi Balozi wa Comoro nchini Iran alizaliwa na kukulia katika familia ya kidini. Alipata masomo yake katika madrassa za Kiarabu na Kiislamu pamoja na shule za Kifaransa nchini Comoro kabla ya kuelekea katika Chuo Kikuu cha Al Azhar nchini Misri alipofanikiwa kuendelea na masomo ya juu. 328910