Ayatullah Sayyid Muhammad Said al-Hakim, mmoja wa wanazuoni na marja' mashuhuri wa Iraq amesema kuwa, kufahamu ukweli na uhakika na wakati huohuo kujiweka mbali na batili kunategemea kunufaika na urithi wa Ahlul Beit (as) au kwa ibara nyingine Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw).
Akizungumza siku ya Alkhamisi huko katika mji mtakatifu wa Najaf na wanachuo wa Chuo Kikuu cha Waidhi cha mji mtakatifu wa Kadhimein, Ayatullah Muhammad Said al-Hakim amesema, kutafuta elimu na uhakika ni moja ya neema bora zaidi ambazo Mwenyezi Mungu amewapa waja wake na kwamba mwanadamu anapasa kufanya juhudi za kutumia vyema akili na mantiki yake ili kufikia ukweli na uhakika wa mambo. Ameongeza kuwa, kutambua na kujua vyema urithi tajiri wa Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) na kunufaika ipaswavyo na urithi huo huwaongezea Waislamu maarifa na ujuzi wa itikadi, misingi na thamani za dini yao. Ayatullah Hakim amesisitiza mwishoni mwa mazungumzo hayo juu ya udharura wa kuimarishwa zaidi ushirikiano wa watu wa Iraq katika kulinda maslahi makuu ya taifa hilo na kutaka kuwepo umoja kati ya makundi na mirengo yote ya nchi hiyo. 330017