IQNA

Kufunguliwa kituo cha utafiti wa muujiza wa Qur'ani mjini Makka

11:16 - December 06, 2008
Habari ID: 1716087
Kituo cha utafiti wa muujiza wa kielimu wa Qur'ani kilifunguliwa siku ya Alkhamisi karibu na Masjidul Haram katika mji mtakatifu wa Makka.
Sherehe za ufunguzi wa kituo hicho zilihudhuriwa na Abdallah abdul Aziz al-Muslih, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Muujiza wa Kielimu wa Qur'ani Tukufu na Sunna za Mtume (saw). Amesema kituo hicho kitashughulikia ukusanyaji wa utafiti na uchunguzi wa muujiza wa kielimu wa Qur'ani Tukufu. Katibu mkuu huyo ameongeza kwamba, idadi kubwa ya wataalamu na watafiti wa Qur'ani watashughulika katika kituo hicho na kusimamia shughuli za utafiti na uchunguzi wa kielimu kuhusiana na muujiza wa Qur'ani katika nchi mbalimbali za dunia. Abdallah al-Muslih amesisitiza kwamba, kuna wasomi na watafiti wengi duniani ambao wana hamu kubwa ya kutalii na kufanya utafiti zaidi kuhusiana na suala la muujiza wa Qur'ani na Sunna za Mtume (saw). Ameongeza kuwa kufahamu uhakika na muujiza wa kielimu wa Qur'ani katika zama hizi na kuufahamishia vijana, ni jambo muhimu ambalo linaweza kuwalinda dhidi ya hatari ya kutumbukia kwenye mtego wa fitina na upotofu wa kifikra na kimaadili.
Katibu mkuu huyo mwishowe amewataka Waislamu kusoma na kuzingatia aya za Qur'ani Tukufu na hivyo kupata kufahamu vyema maana na mafundisho ya kitabu hiki cha Mwenyezi Mungu pamoja na misingi yenye thamani kubwa ya sira na sunna za Mtukufu Mtume (saw). 330038
captcha