IQNA

UNESCO yamuenzi Mfaransa anayetetea haki za wananchi wa Palestina

11:42 - December 13, 2008
Habari ID: 1718428
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO Koichiro Matsuura amempongeza Balozi wa zamani wa Ufaransa katika Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa Stephane Hessel kwa machango wake mkubwa katika kuwatetea wananchi wanaodhulumika wa Palestina.
Matsuura ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa kumuenzi Stephane Hessel uliofanyika mjini Paris, Ufaransa amesema kuwa UNESCO imetenga zawadi ya Kutetea Haki za Binadamu ambayo hutolewa kila baada ya miaka miwili kwa wanaharakati wa haki za binadamu ili kuimarisha utamaduni wa kulinda na kutetea hadhi ya mwanadamu. Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO amesema, mwaka huu Kamati ya Majaji wa Haki za Binadamu ya UNESCO imemteuwa Stephane Hessel kwa ajili ya zawadi hiyo.
Hessel mwenye umri wa miaka 91 alishiriki katika kubuniwa Tangazo la Kimataifa la Haki za Binadamu miaka 60 iliyopita. Tangazo hilo lilipasishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1948.
Mwanadiplomasia huyo mkongwe ametoa hotuba nyingi za kupinga vitendo vya kikatili na mauaji ya Israel dhidi ya wananchi wa Palestina. Daima amekuwa akitetea haki za raia wa Palestina na kutoa wito wa kuundwa dola huru la Palestina mji mkuu wake ukiwa Baitul Muqaddas. 332715

captcha