IQNA

Nembo ya ufunguo wa Quds yakabidhiwa rais wa Tunisia

11:36 - December 14, 2008
Habari ID: 1718844
Muhammad Hussein, Mufti wa Palestina na Taisir at-Tamimi, Kadhi Mkuu wa nchi hiyo wamemkabidhi Rais Zeinul Abedin bin Ali wa Tunisia nembo ya ufunguo wa Quds Tukufu kutokana na uungaji mkono wake kwa Wapalestina katika ngazi za kieneo na kimataifa.
Sherehe za kukabidhiwa nembo ya ufunguo huo pamoja na tawi la mzeituni uliopandwa katika ardhi ya Quds na Msikiti wa al-Aqsa kwa rais huyo zilifanyika huko mjini Tunis kwa mnasaba wa kutangazwa azimio la kimataifa la haki za binadamu. Rais Zeinul Abedin amesema katika sherehe hizo kwamba, umoja wa Wapalestina ni silaha muhimu ya wananchi wa nchi hiyo katika kukabiliana na maghasibu wa Kizayuni. Amesema kuwa mashambulio ya mara kwa mara yanayofanywa na askari wa Israel dhidi ya Wapalestina yamelenga kulifanya eneo la Quds, na hasa Msikiti wa al-Aqsa kuwa la utambulisho wa Kiayahudi. Amesisitiza kuwa kujengwa kwa hekalu la Mayahudi karibu na Msikiti wa al-Aqsa pamoja na ujenzi wa ukuta wa kibaguzi katika maeneo ya Wapalestina ni jinai na ukiukaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu kuwahi kushuhudiwa katika zama hizi dhidi ya jamii ya mwanadamu. Rais Zeinul Abedin bin Ali Ameyataka mashirika na jumuiya za kimataifa kufanya juhudi za kutetea haki za Wapalestina na kusaidia katika kuundwa taifa lao huru pamoja na kuwarudisha wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi zao kwa mujibu wa maazimio na sheria za kimataifa. Wakizungumza katika sherehe hizo, Mufti na Kadhi Mkuu wa Wapalestina pia wameitaka jamii ya kimataifa kutoa mashinikizo zaidi dhidi ya Israel ili kuilazimisha kusimamisha mara moja mashambulio yake ya kinyama na pia kukanyaga haki za kimsingi kabisa za wananchi wasio na hatia wa Palestina. 333098
captcha