IQNA

Umoja wa Ulaya waipiga marufuku filamu ya Fitna

10:56 - December 23, 2008
Habari ID: 1721864
Umoja wa Ulaya umetoa azimio ukipiga marufuku filamu inayokivunjia heshima kitabu kitukufu cha Qur’ani ya Fitna katika nchi wanachama wa umoja huo.
Azimio hilo linasisitiza kuwa: Kuonyeshwa filamu ya Fitna kunawakera na kuwakasirisha Waislamu na kutishia maisha ya amani na usalama kati ya wafuasi wa dini mbalimbali.
Uamuzi huo wa Umoja wa Ulaya umechukuliwa kufuatia ombi lililotolewa na kiongozi wa chama chenye misimamo mikali nchini Uingereza cha United Kingdom Independence Party Nigel Farage aliyemtaka mtengenezaji wa filamu hiyo Geert Wilders kuonyesha filamu ya Fitna nchini Uingereza.
Tarehe 17 mwezi huu wa Disemba pia Umoja wa Ulaya ulipinga kuonyeshwa filamu hiyo inayokitusi kitabu cha Qur’ani katika makao makuu ya bunge la umoja huo mjini Strasbourg, Ufaransa.
Mtengenezaji wa filamu ya Fitna Geert Wilders ambaye ni mbunge mwenye misimamo ya kuchupa mipaka wa Uholanzi na kiongozi wa chama chenye misimamo ya kibaguzi cha Uhuru, alionyesha kwa mara ya kwanza filamu hiyo mwaka jana katika mtandao wa intaneti na kuzusha wimbi la malalamiko na hasira kubwa kati ya Waislamu kote duniani. 336868

captcha