IQNA

Vita vya Gaza vimeimarisha umoja wa Wapalestina

11:02 - January 01, 2009
Habari ID: 1725887
Mashambulio ya kinyama yanayotekelezwa na utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza dhidi ya watu wasio na hatia yamepelekea Wapalestina na walimwengu kwa ujumla kuuchukia zaidi utawala huo, na hata makundi ya Kipalestina ambayo awali yamekuwa na hitilafu kubwa pamoja na mivutano, kuanza kushirikiana na kuimarisha umoja wao.
Hayo yamesemwa na Hussein Ruivaran, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati, ambaye amesema kuwa mashambulio dhidi ya Ukanda wa Gaza yameanzishwa na Wazayuni kwa ajili ya kuivunja kabisa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, lakini kwamba lengo hilo halitafikiwa kwa sababu kufuatia hujuma hiyo ya Wazayuni, Wapalestina wote wameungana na kuwa kitu kimoja. Amesema, Wapalestina wote sasa wanaichukulia Israel kuwa adui wao wa pamoja, na kwa hivyo hata wale waliokuwa wakiichukia Hamas hivi sasa wanashirikiana nayo kwa karibu kwa lengo la kukabiliana na adui Mzayuni, ili kuwalinda Wapalestina kutokana na hujuma ya kinyama ya utawala haramu wa Israel. Ruivaran amaesema kuwa, utawala haramu wa Israel umeanzisha hujuma yake ya kinyama dhidi ya Ukanda wa Gaza ukidhani kwamba ungeweza kuudhibiti ukanda huo katika muda usio mrefu, lakini kwa sasa hali ya mambo haiuruhusu tena utawala huo kufikia lengo hilo. Mtaalamu huyo wa masuala ya Mashariki ya Kati amaesema kwamba, hali ya Israel sasa ni ya mgogoro na kwamba sababu kuu ya mgogoro huo ni kupatikana makundi na harakati za mapambano ya wananchi katika nchi za Lebanon na Palestina. Amesema, utawala haramu wa Israel umeshindwa kabisa kujikwamua na hali hiyo na ndio maana mara kwa mara umekuwa ukitangaza usitishaji vita na harakati hizo ili upate mwanya wa kujiondoa katika hali hiyo ya kuaibisha. Amesema katika vita vya siku 33 vya Lebanon Utawala wa Israel ulipata somo muhimu nalo ni kuwa kushirikishwa wananchi katika mapambano kuna umuhimu mkubwa katika ushindi wa vita na kwa hivyo unajaribu hivi sasa kuwatenganisha wananchi na serikali za Kiarabu ili kuzuia kuwepo kwa ushirikiano na serikali hizo na hivyo kuzitumia katika kuwakandamiza wananchi na hatimaye kuyadhoofisha mapambano yao dhidi ya wavamizi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina. 340557
captcha