IQNA

Shirika la Msamaha Duniani lakosoa msimamo wa Marekani kuhusiana na mauaji ya Gaza

10:29 - January 04, 2009
Habari ID: 1726889
Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International, limekosoa msimamo usiokuwa wa kiuadilifu na wa kibaguzi wa Marekani kuhusiana na mauaji yanayofanywa na Israel huko katika Ukanda wa Gaza na kutoa mashinikizo dhidi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas.
Katika ripoti yake iliyotoa tarehe 4 Januari huko Geneva, shirika hilo limesema kuwa inashangaza kuona kwamba Marekani inazichukulia jinai na mauaji ya kinyama yanayofanywa na Israel dhidi ya wakazi wasio na hatia wala ulinzi huko Gaza, kuwa ni ya kujilinda na huku ikiilaumu Hamas kuwa ndiyo inayopelekea Israel kufanya mashambulio hayo dhidi ya wakazi wa Gaza. Limesema, uungaji mkono huo wa Marekani umehatarisha mno hali ya Gaza na kwamba kuna uwezekano mkubwa wa eneo hilo kushuhudia janga na maafa makubwa ya kibinadamu katika siku zijazo.
Amnesty International imeelezea katika ripoti hiyo wasiwasi wake mkubwa kuhusiana na hatua ya Marekani ya kuupa utawala haramu wa Israel silaha za kisasa kabisa zinazotumiwa na utawala huo katika kuwakandamiza Wapalestina.
Katika kipindi cha siku nane zilizopita za mashambulio ya kinyama ya Wazayuni dhidi ya wakazi wa Gaza, idadi kubwa ya watoto, wanawake na wazee wasio na hatia wameuawa katika Ukanda huo. Marekani imetakiwa na ripoti hiyo kusimamisha mara moja utumaji wa silaha kwa utawala huo na kuulazimisha ufungue mara moja vivuko vya Gaza ili kuruhusu kuingizwa katika ukanda huo misaada ya dharura ya kibinadamu na pia kuandaliwa uwanja wa kupelekwa majeruhi wa mashambulio ya Wazayuni katika hospitali zilizo nje ya ukanda huo. 342751
captcha