Tokea wakati wa kuasisiwa kwake hadi leo, taasisi za kimataifa zimethibitisha wazi mfungamano na upendeleo wao kwa utawala haramu wa Israel kwa kulinda kwa njia yoyote ile maslahi haramu wa utawala huo na Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati. Katika mgogoro wa hivi sasa pia, taasisi hizo zimethibitisha kwa mara nyingine kuwa zinafungamana vilivyo na utawala huo kwa madhara ya Wapalestina ma mataifa yote ya Mashariki ya Kati.
Akizungumzia suala hilo, Ali Asghar Iranmanesh, Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Yemen amesema kuwa taasisi hizo zinazofungamana na kuyategemea madola makubwa duniani, ziko tayari kushirikiana na watenda jinai wakuu ulimwenguni kwa lengo la kulinda maslahi yao, na ndio maana zimeamua kukaa kimya kuhusiana na jinai zinazotekelezwa hivi sasa na Wazayuni huko katika Ukanda wa Gaza. Iranmanesh ameyafananisha mauaji yanayotekelezwa hivi sasa na Wazayuni huko Gaza na yale ya siku 33 nchini Lebanon na kusema kuwa, hatimaye watakaoshindwa katika jinai hizo ni Wazayuni na waungaji mkono wao wa Magharibi. Amesema kuwa nchi hizo za Magharibi hazitaacha kuunga mkono jinai za Wazayuni dhidi ya watu wasio na hatia hadi pale utawala haramu wa Israel utakaposhindwa kabisa na kudhalilishwa kwa mara nyingine tena katika uchokozi wake huko Gaza.
Ameendelea kusema kuwa, kama ungekuwepo umoja na ushirikiano miongoni mwa nchi za Kiarabu na Kiislamu bila shaka utawala haramu wa Israel haungekuwa unatekeleza jinai kama hizi unazozitekeleza dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Ukanda wa Gaza.
Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesikitishwa mno na kimya cha baadhi ya nchi za Kiarabu kuhusiana na jinai za Wazayuni huko Gaza na kusema kuwa kimya hicho bila shaka kinatokana na ujahili na itikadi potofu za baadhi ya watu wanaodai kuwa ni wanazuoni wa Kiislamu pamoja na uchu wa madaraka wa watawala wa nchi hizo wa kuendelea kuhodhi madaraka kwa madhara ya umma mzima wa Kiislamu. 346005