IQNA

Gazeti la Kizayuni: Israel imeshindwa katika vita vya Gaza

9:23 - January 20, 2009
Habari ID: 1733295
Gazeti la Kizayuni la Yediot Ahronot limekiri kwamba utawala haramu wa Israel umeshindwa vibaya katika vita vyake vya kichokozi huko katika Ukanda wa Gaza. Gazeti hilo limesema kwamba utawala huo umeshindwa kabisa kufikia malengo uliyoyaainisha kabla ya kuanzisha vita dhidi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas.
Gazeti hilo limesema kuwa picha ambayo imebaki katika fikra za waliowengi duniani baada ya kumalizika vita vya utawala huo huko Gaza ni ya mauaji ya umati dhidi ya wanawake na watoto na kusisitiza kwamba, suala hilo sio ushindi kwa Israel.
Gazeti hilo limeandika kuwa, lengo la vita hivyo lilikuwa ni kubadili hali ya usalama katika eneo la kusini mwa Ukanda wa Gaza na kuiharibu kabisa Hamas, lengo ambalo halijatimia kabisa baada ya kumalizika vita hivyo. Limeendelea kuandika kuwa, matamshi yaliyotolewa na Ehud Olmert na Ehud Barak, Waziri Mkuu na Waziri wa Vita wa Utawala huo kwamba jeshi la Isral limefikia malengo yake yote huko Gaza ni ya kushangaza mno.
Gazeti jingine la Utawala haramu wa Israel la Maariv pia limekosoa namna mashambulio hayo ya kinyama yalivyoendeshwa na kusema kuwa picha za wanawake na watoto wadogo kuuawa kinyama katika mashambulio hayo hazitafutika katika fikra za waliowengi duniani na kwamba mashambulio hayo yameuharibia jina utawala huo na kuufanya uchukiwe katika ngazi za kimataifa.
Maariv limesisitiza kwamba, mashambulio hayo hayakuzikinaisha fikra za waliowengi kwamba yalifanyika kwa ajili ya kukabiliana na harakati ya Hamas, inayotuhumiwa na utawala huo haramu kuwa ni ya kigaidi.
Gazeti hilo limemaliza kwa kusema kuwa, walimwengu daima watakuwa wakijiuliza swali kwamba, ni kwa nini jeshi la utawala wa Israel liliwaua kwa umati watoto wa Gaza kwa ajili ya kuwalinda watoto wa Israel? 350874
captcha