Ekmeleddin Ihsanoglu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC, amevitaka vyombo vya upashaji habari vya nchi za Kiislamu kuwafichulia walimwengu uchokozi pamoja na jinai za kivita zinazotekelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia huko katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Akizungumza katika kikao cha nane cha Mawaziri wa Habari wa nchi za Kiislamu huko Rabat nchini Morocco, Ihsanoglu, amesema kuwa utawala haramu wa Israel umekuwa ukitekeleza siasa za kiuadui za kufuta kabisa utambulisho wa Wapalestina huko katika mji mtakatifu wa Baitul Muqaddas, na kwamba vyombo vya habari vya ulimwengu wa Kiislamu vina jukumu zito la kufichua njama hatari za utawala huo dhidi ya ulimwengu wa Kiislamu.
Amezungumzia umuhimu wa kuimarishwa Shirika la Kimataifa la Habari la Umoja wa Nchi za Kiislamu (IINA) na kuongeza kuwa katika hali ya hivi sasa, wataalamu wa masuala ya habari wa OIC wanashughulikia suala la hati ya upashaji habari ya shirika hilo.
Akiashiria hali ya kutisha ya maafa ya kibinadamu inayotawala katika Ukanda wa Gaza kutokana na jinai za kivita za utawala wa Israel katika eneo hilo, Ihsanoglu amesisitiza kwamba vyombo vya habari vya nchi za Kiislamu vina jukumu la kufichua utambulisho wa jinai na mauaji wa utawala huo dhidi ya watu wasio na ulinzi, kwa sababu utawala huo umekiuka haki nyingi za kibinadamu na thamani za kiutu katika mashambulio yake ya hivi karibuni katika Ukanda wa Gaza.
Katibu Mkuu huyo hatimaye amesisitiza juu ya kuanzishwa mfuko wa uwekezaji katika miradi ya upashaji habari na vyombo vya habari vya Kiislamu kwa ajili ya kuwafikishia walimwengu sauti ya ulimwengu wa Kiislamu.
Kikao cha nane cha Mawaziri wa Habari wa Umoja wa Nchi za Kiislamu OIC kilianza siku ya Jumanne huko Rabat, kwa usimamizi wa Katibu Mkuu wa OIC na Mfalme Muhammad wa VI wa Morocco. 355573