IQNA

Kuhuishwa utamaduni wa Kiislamu lengo kuu la Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran

11:43 - February 01, 2009
Habari ID: 1738243
Watu wa Iran ambao walikuwa na wangali wana asili ya Uislamu, walinufaika na kiongozi mkubwa na muhimu katika historia ya mwanadamu Imam Khomeini (MA) kwa ajili ya kukabiliana na utamaduni wa Magharibi na kurejesha utamaduni wao wa asili wa Kiislamu.
Akizungumza na shirika la habari la Iqna, Muhammad Aali Basiri, Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu nchini Senegal amesema kuwa wananchi wa Iran ambao taratibu walikuwa wanapoteza utambulisho wao halisi wa Kiislamu na kuukumbatia utamaduni wa Magharini kutokana na uongozi mbovu wa Shah wa Iran, ghafla walipata fursa ya kuuhuisha utambulisho na utamaduni wao kupitia uongozi shupavu wa Ayatullah Imam Khomeini (MA).
Amesema kuwa, Imam Khomeini (MA) ambaye ndiye mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, daima alikuwa akisisitiza umuhimu wa kuzingatiwa utamaduni wa Kiislamu katika jamii kutokana na umuhimu wake wa kulea jamii iliyo salama. Ameongeza kuwa, jambo hilo pia limeanza kuzingatiwa na mataifa mengi duniani ikiwemo Marekani katika utawala mpya wa Rais Barrack Obama, ambaye amesisitiza kuleta mabadiliko ya kiutamaduni nchini humo akisema kuwa mabadiliko ya kijeshi na kiviwanda hayatoshi kulinda maslahi ya nchi.
Basiri ameendelea kusema kuwa, Obama anaamini kuwa fikra za nguvu za kijeshi na kiviwanda tu hazina tena nafasi katika ulimwengu wa leo na kwamba marekebisho ya kiutamaduni na kidemokrasia ndiyo yanayopasa kupewa umuhimu, jambo ambalo taifa la Iran lililigundua mapema miaka 30 iliyopita na kusimama peke yake duniani katika kukabiliana na dhulma liliyotwishwa na nchi za Magharibi ulimwenguni, zilizoliwekea kila aina ya vikwazo vya kiuchumi na kisiasa. Kwa kutekeleza siasa hizo mbovu za vikwazo, madola hayo ya Magharibi yalikuwa na lengo la kuuangusha mfumo mchanga wa Kiislamu nchini, jambo ambalo halikufanikiwa. Huku akiashiria njama za nchi za Magharibi katika miaka ya hivi karibuni za kuharibu utamaduni wa nchi za Kiislamu na hasa nchini Iran, Basiri amesema kuwa nchi za Magharibi zimetambua kwamba hujuma ya kiutamaduni ndiyo njia bora zaidi ya kufikia malengo yao katika ulimwengu wa Kiislamu, kinyume na zilivyokuwa zikifanya huko nyuma ambapo zimekuwa zikitegemea zaidi mashinikizo ya kijeshi na kisiasa. 356339
captcha