IQNA

Wanafikra wawasilishe uvumbuzi wa kuimarisha uhusiano miongoni mwa dini

12:03 - February 18, 2009
Habari ID: 1745472
Washiriki wa kikao cha sita cha Marekani na Ulimwengu wa Kiislamu huko Doha mji mkuu wa Qatar wametoa taarifa wakiwataka wanafikra wa dunia kuwasilishia njia za uvumbuzi wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano miongoni mwa wafuasi wa dini mbalimbali.
Gazeti la as-Sharq limeandika kwamba taarifa hiyo ya mwisho ya kikao Doha imetaka kuwepo heshima ya pande mbili, juhudi za kuleta uadilifu ulimwenguni na kufanyika mazungumzo yenye nia njema kati ya Marekani na ulimwengu wa Kiislamu na hasa katika masuala yanayohusiana na Iran na Afghanistan.
Washiriki wametaka mazungumzo na ushirikiano uimarishwe kati ya Marekani na Ulimwengu wa Kiislamu na kutafuta njia za kuimarisha amani, usamehevu na maelewano kati ya nchi mbili. Wanafikra na wasomi walioshiriki katika kikao hicho cha Doha pia wametoa wito wa kuzingatiwa misingi ya pamoja ya dini za mbinguni na kuondoa changamoto pamoja na vizuizi vinavyozuia kuwepo ushirikiano kati ya Marekani na Ulimwengu wa Kiislamu.
Mkuu wa Taasisi ya Brookings ya nchini Marekani amesema kuwa, lengo la kikao hicho si kuwasilishwa fikra tupu bila ya kuzifanyia kazi, bali mipango ya kivitendo inapaswa kutekelezwa na wanafikra wa pande mbili pamoja na mashirika ya kidini ulimwenguni kwa madhumuni ya kuondoa hali a kutoaminiana kati ya pande hizi. Amesema kufikia sasa, taasisi hiyo imewasilisha na kutekeleza mipango mingi kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa pande mbili ikiwemo ya kiutamaduni, kielimu na kimafunzo.
Kikao hicho cha siku tatu kilichoanza Jumamosi tarehe 14 Februari kimewajumuisha wataalamu wa masuala mbalimbali ya kielimu, biashara, siasa, vyombo vya habari, uchumi, utafiti, dini na wanaharakati wa jumuiya za kiraia.
Kuchunguzwa masuala ya kiutamaduni ya ulimwengu wa Kiislamu, mivutano kati ya Waarabu na utawala haramu wa Israel, mgogoro wa kiuchumi, udhamini wa nishati katika karne ya 21 na athari ya uongozi wa Rais Barack Obama wa Marekani kwa ulimwengu wa Kiislamu ni miongoni mwa masuala ambayo yamejadiliwa katika kikao hicho. 365198
captcha