Askari usalama wa Saudi Arabia wanaolinda makaburi ya Baqii, walikozikwa watukufu na viongozi wa Kiislamu mjini Madina, Ijumaa alasiri waliwafukuza Waislamu waliokuwa wamekwenda kuyazuru makaburi hayo na kuwatia nguvuni watano miongoni mwao.
Kwa mujibu wa gazeti la Saudia la Ukadh, Waislamu 500 walikuwa wamekusanyika katika eneo hilo kwa lengo la kufanya ziara katika makaburi hayo lakini walizuiwa na askari usalama.
Kwa mujibu wa madai ya gazeti hilo, pamoja na kuwa Waislamu hao walikuwa wamefahamishwa kwamba wakati wa kuyazuru makaburi hayo ulikuwa umekwisha, lakini waliendelea kukusanyika pembeni ya makaburi hayo na kupiga mayowe, kuasi na hata baadhi yao kufanya juhudi za kuwashambulia askari wanaolinda makaburi hayo.
Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti hilo baada ya kuona hivyo, askari hao waliwajibika kuchukua hatua ya kuwatawanya Waislamu hao na kuwatia nguvuni watano miongoni mwao. Baadaye Waislamu hao walipelekwa katika kituo maalumu cha polisi ili kuhojiwa. 366997