Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu watafanya kikao cha dharura mjini Cairo, Misri, tarehe 5 Mei kwa lengo la kujadili suala la Quds Tukufu na ufikishaji misaada kwa wananchi madhlumu wa Palestina.
Kikao hicho kitafanyika kutokana na ombi la wakuu wa Palestina kwa ajili ya kuchunguza matukio na hali ya hivi karibuni kabisa huko Quds Tukufu na vilevile juhudi za utawala haramu wa Israel za kubadili muundo wa kijamii wa eneo hilo takatifu kwa maslahi ya Mayahudi. Mawaziri hao wameazimia kutafuta njia za kukabiliana na njama za utawala haramu wa Israel za kulifanya eneo la Quds Tukufu kuwa la Mayahudi na kufuta kabisa utambulisho wa Kiislamu na Kiarabu wa eneo hilo na vilevile kujadili njia za kuwafikishia misaada ya kibinadamu wakimbizi wa Kipalestina wanaoishi katika eneo hilo.
Hivi karibuni Amr Musa, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu alipokea barua kutoka kwa Riadh al-Maliki, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina akimbainishia njama za uharibifu na ukandamizaji zinazotekelezwa na utawala haramu wa Israel huko katika Ukanda wa Gaza na Quds Tukufu na kuitaka jumuiya hiyo ichukue hatua za dharura kwa lengo la kukabiliana na uharibifu huo wa Wazayuni katika maeneo matakatifu ya Kiislamu na pia njama zake za kufuta utambulisho wa Kiislamu na Kiarabu huko Quds na kuufanya kuwa wa Kiayahudi.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu pia amelaani kitendo cha magenge ya walowezi wa Kizayuni cha kushambulia Msikiti wa al-Aqsa na kusema kuwa jambo hilo linabainisha wazi utambulisho halisi wa kijinai na kigaidi wa utawala wa Irael. Amesema njama za utawala huo za kufanya mji wa Quds kuwa wa Kiyahudi zinapasa kusimamishwa mara moja na kwamba utekelezaji wake unazidi kuharibu uwezekano wa kufanyika mazungumzo eti ya amani kati ya pande mbili hizo. 391407