IQNA

Uhuru wa dini kupitia fiqhi ya Kiislamu kuchunguzwa katika kikao cha Sharja

16:00 - April 30, 2009
Habari ID: 1771859
Katika siku ya pili ya kikao chao huko Sharja nchini Imarati, wanazuoni na wataalamu wa masuala ya fiqhi ya Kiislamu wapatao 250 wanaoshiriki katika duru ya 19 ya Baraza la Fiqhi ya Kiislamu, wamejadili masuala matatu muhimu ambayo ni uhuru wa kidini, uhuru wa kusema na adhabu ya watu wanaoritadi, kupitia fiqhi ya Kiislamu.
Kwa mujibu wa gazeti la al-Madina, miongoni mwa wanazuoni mashuhuri ambao hawakushiriki katika duru hii ya kikao hicho ni Yusuf Qardhawi, Ali al-Qura Daghi, mwandishi na mtafiti wa Kikurdi anayeishi nchini Qatar, Taha Jabir al- Ulwani, mkuu wa zamani wa Baraza la Sheria za Kiislamu katika eneo la Amerika Kaskazini na Ali as-Salus, mhadhiri wa masuala ya fiqhi katika chuo kikuu cha Qatar.
Washiriki wa kikao hicho wamesisitiza juu ya umoja miongoni mwa Waislamu na kuongeza kuwa heshima na thamani ya umma wa Kiislamu ni kubwa zaidi na isiyoweza kukandamizwa na nchi za Magharibi. Wamesema kuwa thamani za kidini hazipaswi kutusiwa na nchi hizo kwa kisingizio cha uhuru wa kusema na kwamba uhuru wa kidini na kijamii unapaswa kutekelezwa katika misingi ya heshima ya pande mbili.
Kikao hicho cha 19 cha Baraza la Fiqhi ya Kiislamu kilianza siku ya Jumapili huko Imarati chini ya anwani ya 'Haki za Binadamu katika Mazingira Yanayofaa na Salama' na kinatazamiwa kumalizika hii leo Alkhamisi. 396832
captcha