Akizungumzia suala hilo hapo jana Jumamosi mbele ya waandishi habari huko Quds, Abdul Qadir amesema kuwa watawala wa Israel wametupilia mbali ombi la viongozi wa Palestina la kuwataka wawarejeshee jiwe hilo la kale la Msikiti wa al-Aqsa ambalo linahusiana na kipindi cha watawala wa Umawi. Amesema kuwa viongozi wa Palestina wana nia ya kuwashtaki mahakamani na pia katika Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa Unesco, watawala wa Israel kuhusiana na wizi huo wa athari za kale na za kihistoria katika Msikiti wa al-Aqsa. Amesema, mashtaka hayo yatatimia katika fremu ya masuala ya kisiasa, kisheria na kipropaganda.
Abdul Qadir amesema kuwa Wapalestina watalitaka shirika la Unesco kuushinikiza utawala huo kurejesha jiwe hilo kwa kulitaka litume mwakilishi wake katika vikao vya mahakama itakayoendesha kesi kuhusiana na kadhia hiyo. Amesisitiza kwamba, Wapalestina kamwe hawatalegeza msimamo wao wa kutaka kurejeshewa jiwe hilo la kihistoria na la kale la Msikiti wa al-Aqsa kwa sababu kufanya hivyo kutawashajiisha Wazayuni kuendelea kuiba athari za kale za msikiti huo mtukufu.
Yapata mwezi mmoja uliopita, Idara ya Wakfu ya Kiislamu ya Quds Tukufu ilitangaza kwamba Wazayuni waliingia katika msikiti huo na kuiba jiwe hilo la kale lililokuwa katika eneo la kusini mashariki mwa Msikiti wa al-Aqsa na kisha kuliweka katika uwanja wa hekalu la Mayahudi. 398219