Maonyesho ya vitabu vya kidini, kuitamaduni, kijamii, kifasihi, kielimu na vinavyotumika katika vyuo vikuu yamepokelewa kwa wingi na wananchi wa Iraq katika mji mtakatifu wa Karbalaa.
Abbas Dhiyaiyan, msimamizi wa Kiirani wa maonyesha hayo yanayomalizika leo Jumamosi amesema kuhusiana na suala hilo kuwa zaidi ya vitabu laki mbili na nusu vilivyo na zaidi ya nwani alfu 10 vilitazamwa na kukaguliwa na zaidi ya Wairaki laki moja. Ameongeza kuwa mbali na maonyesho ya vitabu katika nyanja zilizotajwa maonyesho hayo pia yalihusisha CD na sanaa za mikono. Amesema asilimia 70 ya vitabu vilivyoonyeshwa katika maonyesho hayo vilikuwa katika lugha ya Kiarabu, asilimia 20 katika lugha ya Kiingereza na asilimia 10 katika lugha ya Kifarsi. Amesema kuwa kwa wastani kila siku watu 20,000 wameyatembelea maonyesho hayo. Amekumbusha kwamba maonyesho hayo yameandaliwa kutokana na wito uliotolewa na idara inayosimamia haramu takatifu za Imam Hussein na Hazarat Abbas (AS) na kwamba maonyesho yajayo ya vitabu vya Iran nchini Iraq yatafanyika katika mji wa Basra.
Tunakumbusha hapa kuwa maonyesho hayo ya vitabu ya Haramein mjini Karbalaa yanayomalizika leo tarehe 7 Agosti yalizinduliwa mjini humo siku ya Jumatatu tarehe Pili Agosti.
627935