IQNA

Qibla ya Pamoja inapaswa kuwa chanzo cha "Umoja wa Kweli,” asema mwanazuoni wa Malaysia

18:38 - September 23, 2025
Habari ID: 3481275
IQNA – Mwanazuoni na mwanaharakati kutoka Malaysia ametoa wito kwa Waislamu kote duniani kuonesha mshikamano kwa vitendo badala ya maneno, akisisitiza kuwa Qibla ya pamoja inapaswa kuwa msingi wa mshikamano wa Ummah.

Mohammad Azmi Abdul Hamid, Rais wa Baraza la Mashauriano la Mashirika ya Kiislamu Malaysia (MAPIM), alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA)  pembezoni mwa Mkutano wa 39 wa Umoja wa Kiislamu uliofanyika Tehran mapema mwezi Septemba.

Alieleza kuwa ulimwengu wa Kiislamu unahitaji sauti ya pamoja yenye nguvu ili kutetea Palestina na jamii nyingine zinazodhulumiwa. Alitaja Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kama jukwaa lenye uwezo mkubwa, lakini akasisitiza kuwa linahitaji kufanyiwa mageuzi ili liwe chombo chenye ufanisi zaidi.

“Msingi muhimu zaidi wa umoja miongoni mwa wafuasi wa madhehebu mbalimbali ya Kiislamu ni Qibla moja, yaani wote huswali kuelekea mwelekeo mmoja,” alisema Azmi.

Aliwahimiza viongozi wa nchi zenye Waislamu wengi kuacha kutegemea Umoja wa Mataifa pekee, na badala yake kujenga miungano mbadala kupitia taasisi kama OIC, Harakati ya Kutofungamana, ASEAN, na BRICS ili kuweka shinikizo kwa madhalimu.

Aidha, alitoa wito wa kuanzishwa kwa mtandao huru wa vyombo vya habari vya Kiislamu ili kukabiliana na propaganda za Kizayuni na za Magharibi.

Alisisitiza kuwa nchi za Kiislamu “zinapaswa pia kusaini mkataba madhubuti wa ulinzi na usalama ili kuzuia uvamizi, kuratibu mikakati ya pamoja ya ulinzi, na kushirikiana kwa karibu katika nyanja za kiuchumi, hasa katika sekta muhimu kama vile nishati, usalama wa chakula, na teknolojia.”

Azmi aliongeza kuwa mageuzi ya OIC na kuonesha mshikamano kwa hatua madhubuti kama vile kususia na vikwazo ni hatua muhimu za kuimarisha Ummah wa Kiislamu na kuonesha nafasi yake katika masuala ya kimataifa.

“Dhamiri ya Dunia Imeamka”

Kuhusu hali ya kibinadamu huko Gaza, Azmi alisifu juhudi za kimataifa kama msafara wa Sumud, unaolenga kufikisha misaada na kuhamasisha dunia kuhusu hali ya ukanda huo. Alisema juhudi hiyo inaakisi maadili ya pamoja ya amani, msaada wa kibinadamu, na heshima kwa sheria za kimataifa.

“Juhudi hii ya kipekee inaonesha mwamko wa dhamiri ya dunia mbele ya jinai za utawala dhalimu wa Israeli,” alisema, akiongeza, “Watu wa kawaida kutoka kila pembe ya dunia, wakati serikali nyingi zikifumbia macho janga hili, wamejitokeza kwa matumaini ya kupunguza machungu ya Wapalestina walioumia.”

3494716

captcha