Azimio hilo lililopitishwa kwa kura 142 zilizounga mkono dhidi ya 10 zilizopinga limeidhinisha kile kinachojulikana kama "Azimio la New York", taarifa inayoagiza kutekelezwa suluhisho la kuwepo madola mawili, iliyowasilishwa kwa pamoja na Ufaransa na Saudi Arabia mnamo mwezi Julai mwaka huu.
Nchi zilizoungana na utawala wa kizayuni wa Israel na Marekani kupinga azimio hilo ni Argentina, Hungary, Micronesia, Nauru, Palau, Papua New Guinea, Paraguay na Tonga. Nchi nyingine 12 zilijizuia kupiga kura.
Tangazo hilo la kurasa saba ni matokeo ya mkutano wa kimataifa ulioitishwa katika Umoja wa Mataifa kujadili ukaliaji ardhi kwa mabavu unaoendelea kufanywa kwa miongo kadhaa sasa na utawala ghasibu wa Israel. Marekani na utawala huo wa kizayuni ziliususia mkutano huo wa mwezi Julai.
Azimio la New York ambalo limeitenga harakati ya ukombozi wa Palestina ya Hamas, limetoa wito pia wa kuchukuliwa "hatua ya kivitendo ya pamoja kumaliza vita vya Israel huko Ghaza na kuwepo utekelezaji mzuri wa suluhisho la madola mawili."
Azimio hilo liliidhinishwa pia na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kutiwa saini mwezi Julai na nchi 17 wanachama wa Umoja wa Mataifa, zikiwemo nchi kadhaa za Kiarabu.
Washirika wa muda mrefu wa Magharibi wa utawala wa kizayuni wa Israel, ikiwa ni pamoja na Ubelgiji, Ufaransa, Uingereza, Canada, na Australia, zilitangaza hapo kabla mipango ya kulitambua Dola la Palestina wakati wa vikao vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa vilivyoanza Septemba 8 na kuendelea hadi Septemba 23. Zikichukua hatua hiyo, nchi hizo zitajiunga na mataifa 147 ambayo tayari yanaitambua Palestina kama dola.
Karibu robo tatu ya nchi zote 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa zinalitambua Dola la Palestina lililotangazwa mwaka 1988 na uongozi wa Palestina uliokuweko uhamishoni.
Hayo yanajiri katika hali ambayo waziri mkuu wa utawala wa kizayuni Benjamin Netanyahu alisisitiza siku ya Alkhamisi kwamba utawala huo ghasibu hautaruhusu katu kuwepo Dola la Palestina.
3494571