IQNA

Wanasayansi kutoka India, Uturuki na Iran watunukiwa Tuzo ya Mustafa (SAW) ya Mwaka 2025

14:00 - September 09, 2025
Habari ID: 3481206
IQNA – Wanasayansi watatu mashuhuri ambao ni Mohammad K. Nazeeruddin kutoka India, Mehmet Toner kutoka Uturuki, na Vahab Mirrokni kutoka Iran wametangazwa kuwa washindi wa Tuzo ya Mustafa (SAW) ya mwaka 2025.

Tuzo hiyo imetolewa kwa kutambua mchango wao wa kipekee katika nyanja za seli za jua za perovskite, teknolojia ya kugundua seli adimu kwa kutumia microfluidics, na algorithimu za grafu za kiwango kikubwa.

Katika hafla iliyofanyika tarehe 8 Septemba katika Ukumbi wa Vahdat mjini Tehran, maafisa wa serikali, wasomi, na wanasayansi kutoka ulimwengu wa Kiislamu walikusanyika kwa heshima ya washindi wa Tuzo ya Mustafa (SAW) ya mwaka huu.

Tuzo hizo zilitangazwa rasmi na Mahdi Safarinia, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Mustafa, ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Sera ya Tuzo hiyo. Hotuba ya utangulizi ilitolewa na Profesa Ali Akbar Salehi, Mwenyekiti wa Kamati ya Kisayansi ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran.

Kuhusu Washindi

  • Profesa Mohammad K. Nazeeruddin kutoka India alitunukiwa tuzo katika fani ya Sayansi ya Msingi na Uhandisi kwa ubunifu wake katika teknolojia ya seli za jua za perovskite. Akihutubu, alitoa shukrani kwa walimu wake, wenzake, wanafunzi, taasisi alizosoma, na familia yake kwa mchango wao katika safari yake ya kielimu. Alisisitiza kuwa kazi yake inalenga changamoto muhimu ya nishati safi, na akawahimiza vijana wa Kiislamu kuwa na shauku, azma, na bidii katika taaluma. Profesa Mehmet Toner kutoka Uturuki alipokea tuzo katika Sayansi ya Maisha na Tiba kwa ubunifu wake wa vifaa vya nano/microfluidic vinavyotumika kutenga seli adimu. Akizungumza mbele ya hadhirina, alikumbuka miaka yake ya awali ya masomo katika Chuo Kikuu cha Ufundi cha Istanbul, ambako walimu wawili walimfundisha umuhimu wa kuuliza maswali sahihi. Teknolojia yake ya chip sasa inasaidia katika kugundua saratani na inatumika katika tafiti za afya ya ubongo, urejeshaji wa tishu, na masomo ya mishipa ya fahamu. Profesa Vahab Mirrokni kutoka Iran alitunukiwa tuzo katika Sayansi na Teknolojia ya Mawasiliano na Habari kwa kazi yake ya locality-sensitive hashing na algorithimu za grafu za kiwango kikubwa. Akizungumza kwa lugha ya Kifarsi, alimshukuru baba yake ambaye ni mtaalamu wa hisabati, na mama yake aliyemfundisha kufuata njia ya Mtume Muhammad (SAW). Alisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika utafiti wa kisayansi na akasema kuwa utofauti katika timu za utafiti ni jambo la msingi. Kama mwanasayansi mhamiaji, aliwahimiza wanafunzi kuwa na subira, na kama ilivyo kwa washindi waliopita Ugur Sahin na Omid Farokhzad, alitoa zawadi yake ya fedha kwa mpango wa Medali ya Mwanasayansi Chipukizi.

Mchakato wa Uchaguzi

Katika hafla ya kufunga, Profesa Salehi alieleza mchakato wa uteuzi: kuanzia tangazo la kuwaalia wasomi wawasilishe kazi zao mwezi Februari 2024, kupokea zaidi ya mapendekezo 5,200 katika makundi matatu, hadi orodha fupi ya wagombea 24 waliopitiwa na jopo la wanasayansi 100 wa kimataifa, na hatimaye kuchaguliwa washindi watatu.

Aidha, alitangaza kuwa kwa mara ya kwanza, Medali ya Mwanasayansi Chipukizi imetolewa kwa watafiti watatu kutoka Iran, Malaysia, na Uturuki, ishara ya kuongezeka kwa msisitizo wa tuzo hiyo katika kukuza vipaji vipya.

Kuhusu Tuzo ya Mustafa (SAW)

Tuzo ya Mustafa (SAW), ambayo imepewa jina Mtume Muhamamd Al Mustafa (SAW),  ni tuzo ya sayansi na teknolojia inayotolewa kila baada ya miaka miwili na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Mustafa chini ya mwavuli wa Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu (OIC). Lengo lake ni kutambua mafanikio ya kisayansi yenye athari kwa jamii kutoka ulimwengu wa Kiislamu.

Washindi hupokea zawadi ya fedha, medali, na diploma. Tuzo hii inajumuisha makundi kama vile Sayansi na Teknolojia ya Mawasiliano na Habari; Sayansi ya Maisha na Tiba; Sayansi ya Msingi na Uhandisi; na Sayansi ya Nano na Teknolojia ya Nano. Wanaostahiki ni wanasayansi wa imani yoyote wanaofanya kazi katika nchi za Kiislamu, pamoja na Waislamu popote walipo duniani.

Tuzo ya Sayansi ya Mustafa SAW (The Mustafa (PBUH) Prize) ilizinduliwa mwaka 2013 na kisha ilitolewa mara ya kwanza mwaka 2015 mjini Tehran ambapo wakati huo washindi walikuwa ni Profesa Omar Yaghi wa Jordan, mtaalamu wa nanoteknolojia na Profesa Jackie Ying wa Singapore katika uga wa bio-nanoteknolojia.

Tuzo hiyo hutolewa kila baada ya miaka miwili sambamba na maadhimisho ya Maulid ya Mtume Muhammad Al Mustafa (SAW).

3494533

captcha