Akizungumza katika kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) chini ya anuani ya “Karne 15 za Kumfuata Mjumbe wa Nuru na Rehema”, Sheikh Ghazi Hanina alisema kuwa maisha ya Mtume Muhammad (SAW) hayakuwa kwa Waislamu pekee, bali kwa wanadamu wote na hata viumbe vyote. Akinukuu aya za Qur’ani, alisisitiza kuwa Mtume Muhammad (SAW) alitumwa kama “rehema kwa walimwengu” na mfano wa tabia njema.
Sheikh Hanina alisema: " Mtume Muhammad (SAW) alikuja kumkomboa mwanadamu kutoka utumwa wa kuwatumikia binadamu wenzake na kisha akamuongoza kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu pekee." Ameendelea kusema kuwa uhuru wa kweli unapatikana katika kumwabudu Muumba badala ya kusalimu amri kunyanyaswa au kutumiwa vibaya.”
Alifafanua kuwa ujumbe wa Mtume Muhammad (SAW) ulilenga kuinua hadhi ya mwanadamu, kumpa heshima, uhuru, na mamlaka bila kujali rangi au asili. “Hakuna Mwarabu aliye bora kuliko asiye Mwarabu, wala mweupe kuliko mweusi, isipokuwa katika uchamungu,” alikumbusha kwa kunukuu maneno ya Mtume Muhammad (SAW).
Sheikh Hanina alifungamanisha mafundisho haya na changamoto za kisasa, akieleza kuwa migogoro ya dunia ya leo inaakisi miradi miwili inayoshindana: mmoja unaolenga kuuteka ubinadamu chini ya “mradi wa Kimarekani-Kizayuni-KiMagharibi”, na mwingine unaotaka kumrejesha mwanadamu kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu, kama inavyojidhihirisha katika Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Alisema kuwa ujumbe wa Mtume Muhammad (SAW) pia ulikuwa ni kuwatetea wanyonge. “Uislamu unataka kuwapa heshima na hadhi wale waliodhulumiwa, ambao Marekani na Uzayuni wanataka kuwafanya watumwa na watumiaji tu,” alisema.
Sheikhe huyo aliwakumbusha Waislamu kuwa Mtume Muhammad (SAW) alijitolea maisha yake kuwaongoza watu kwenye imani, akipata upinzani huko Makka kutoka kwa viongozi wa kikabila, na baadaye Madina kutoka kwa wanafiki. Alilinganisha changamoto hizo za kihistoria na hali inayowakabili mataifa ya Kiislamu leo.
Katika kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), Sheikh Hanina aliwahimiza waumini kushikilia misingi ya haki, uwajibikaji, na maadili ya kiroho.
Alihitimisha kwa kusisitiza kuwa ibada kwa Mwenyezi Mungu pekee ndiyo kiini cha uhuru wa kweli. “Kumtumikia Mwenyezi Mungu ni uhuru kamili hapa duniani,” alisema. “Uislamu ni dini ya uhuru, heshima, mamlaka, utukufu, na nguvu.”
3494560