IQNA

Misikiti ya Uskochi yakabiliwa na hatari za hujuma za kigaidi, yaimarisha usalama

13:35 - September 14, 2025
Habari ID: 3481230
IQNA – Misikiti kote Uskochi au Scotland nchini Uingereza imeongeza kwa kiwango kikubwa hatua za kiusalama, ikiwemo kuajiri walinzi binafsi na kuweka ulinzi wa saa 24, kufuatia njama ya kigaidi iliyozimwa na ongezeko la mashambulizi ya chuki dhidi ya Uislamu.

Omar Afzal kutoka Jumuiya ya Misikiti ya Uskochi alisema kuwa “kuna hofu na taharuki kubwa ndani ya jamii.” Akaongeza: “Jamii inajihisi iko katika hatari na hali ya kutokuwa salama. Misikiti kote nchini inatafakari upya hatua zake za kiusalama na kuziboresha.” Misikiti kadhaa tayari imeajiri walinzi binafsi, huku Msikiti Mkuu wa Glasgow , ambao ni mkubwa zaidi Uskochi , ukiwa chini ya ulinzi wa saa 24.

Afzal alisema hatua hiyo inaakisi kuongezeka kwa vitisho katika miezi ya hivi karibuni. Mwezi Machi, kijana mmoja alirusha rangi kwenye msikiti wa Aberdeen na kuvunja dirisha huku waumini wakiwa ndani. Mwezi uliofuata, wahalifu wenye chuki dhidi ya Uislamu walilenga msikiti wa Elgin kwa mara ya tatu, wakiharibu madirisha kadhaa. Hivi karibuni, Kituo cha Kiislamu cha Newton Mearns kiliripoti tukio ambapo mtu mmoja alidaiwa kumshambulia msichana wa shule Mwislamu barabarani na kutoa vitisho dhidi ya jamii hiyo.

Na mwezi Agosti, kijana wa miaka 17 aliyeelezewa mahakamani kuwa “mwenye kupendelea itikadi za Nazi” alihukumiwa kifungo cha miaka 10 kwa kupanga kuchoma Kituo cha Kiislamu cha Inverclyde kilichopo Greenock. Kijana huyo alikuwa amewajengea urafiki waumini ili kupata fursa ya kuingia msikitini kabla ya kupanga mauaji ya halaiki. Afzal alisema: “Kama si hatua ya haraka ya Polisi wa Uskochi, tukio hilo lingegeuka kuwa janga la vifo vingi, shambulizi la kigaidi lililopangwa kutekelezwa katika msikiti huo.” Afzal alionya kuwa hali ya chuki dhidi ya Uislamu inazidi kuwa mbaya. “Hasa kwa kuzingatia mambo ambayo watu sasa wanaweza kusema hadharani kwa urahisi, na jinsi mashambulizi dhidi ya Waislamu, misikiti, na hata hoteli zinazowahifadhi wakimbizi yamekuwa jambo la kawaida. Ni tatizo linalojitokeza kote nchini.” “Tusiendelee kujidanganya hapa Uskochi tukidhani kuwa sisi ni tofauti na yanayotokea Uingereza au Ulaya kwa ujumla.

Tunashuhudia dalili za matamshi yenye sumu kutoka kwa wanasiasa, yanayoakisiwa na vyombo vya habari, yakijitokeza mitaani ambapo masuala halali yanayotolewa na watu yanageuzwa kuwa silaha dhidi ya jamii za wachache na Waislamu.” Aliongeza kuwa uchunguzi wa umma kuhusu chuki dhidi ya Uislamu nchini Uskochi tayari ulitoa mapendekezo ambayo hayajatekelezwa.

“Tumeona hali hii ikija, na nadhani sasa ni wakati wa kuchukua hatua madhubuti na za wazi kukabiliana nayo.” Waziri Mkuu wa Uskochi, John Swinney, alisema: “Vurugu, chuki, ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya Uislamu na Uyahudi havina nafasi katika jamii yetu, na hakuna mtu anayepaswa kukumbwa na vitendo hivyo. Serikali hii itafanya kila juhudi kuhakikisha kila mtu anayeishi Uskochi analindwa, na kwamba tumeungana katika kupinga yeyote anayejaribu kutumia machafuko kama njia ya kugawanya watu.”

Akaongeza: “Uskochi ni jamii yenye utofauti na tamaduni mbalimbali ambapo kila mtu anakaribishwa, na ninataka tuungane kupinga yeyote anayejaribu kutumia vurugu na machafuko kuleta mgawanyiko. Hata hivyo, hatuko salama dhidi ya vitendo vya wachache wenye misimamo mikali na hivyo ni lazima tuendelee kuwa waangalifu.”

3494586 

captcha