Kauli hiyo ilitolewa katika tamko la mwisho la mkutano wa dharura wa kilele wa Kiarabu-Kiislamu uliofanyika Jumatatu mjini Doha. Mkutano huo ulifuatia shambulizi la kombora la Israel lililotokea tarehe 9 Septemba, lililolenga eneo la makazi ambapo viongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, walikuwa wakijadili pendekezo la kusitisha vita lililowasilishwa na Marekani kuhusu mgogoro wa Gaza.
Kwa mujibu wa tamko hilo, shambulizi hilo lilikuwa “kitendo cha kiwoga na kivamizi” na ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya Qatar, likifanyika katika eneo lililotambuliwa kimataifa kama uwanja wa mazungumzo ya upatanishi.
Ingawa viongozi wa juu wa Hamas walinusurika, wanachama watano wa kundi hilo pamoja na afisa mmoja wa usalama wa Qatar waliuawa. Viongozi wa mkutano huo walieleza kuwa mashambulizi hayo yalilenga kuvuruga juhudi za upatanishi na kuzuia hatua za kuelekea kusitisha vita.
Tamko hilo liliitaka dunia kuchukua “hatua za kisheria na zenye ufanisi” kukomesha ukatili wa Israel dhidi ya Wapalestina. Pia lilihimiza mataifa kutathmini upya uhusiano wao wa kidiplomasia na kiuchumi na utawala huo, na kufuatilia uwajibikaji kupitia njia za sheria za kimataifa.
Washiriki wa mkutano huo walionesha mshikamano na Qatar, Misri, na Marekani katika juhudi zao za upatanishi, na wakasisitiza umoja na mshikamano na Doha dhidi ya vitisho vya baadaye. Viongozi hao walisisitiza tena kuunga mkono suala la Palestina, wakilaani vita vya Israel dhidi ya Gaza ambavyo walisema vimesababisha “janga la kibinadamu lisilokuwa na mfano.”
Tamko hilo pia lilikataa vikali jaribio lolote la kuhamisha kwa nguvu Wapalestina au kuteka ardhi iliyokaliwa kwa mabavu, na likatoa wito wa kusitishwa mara moja kwa uvamizi wa Israel. Aidha, taarifa hiyo ilisisitiza umuhimu wa usalama wa pamoja na mshikamano miongoni mwa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu.
Mkutano huo uliwaleta pamoja viongozi kutoka nchi wanachama 57 wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na nchi 22 wanachama wa Jumuiya ya Kiarabu. Qatar imekuwa mpatanishi muhimu katika mazungumzo ya kusitisha vita, sambamba na Misri.
Kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza, zaidi ya Wapalestina 65,000—takriban nusu yao wakiwa wanawake na watoto—wameuawa tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi yake mnamo Oktoba 2023.
3494618