IQNA

Waswasi watanda baada ya Msikiti wa Taunton Uingereza kuvunjwa katika tukio la chuki

16:08 - September 13, 2025
Habari ID: 3481226
IQNA – Kitendo cha kuvunjwa kwa madirisha ya Msikiti wa Taunton, nchini Uingereza, kimezua hasira na huzuni miongoni mwa wanajamii wa eneo hilo, huku polisi wakikitaja tukio hilo kuwa ni uhalifu wa chuki unaochochewa na misingi ya kidini au ya rangi.

Polisi wa Avon na Somerset walithibitisha kuwa madirisha kadhaa ya Msikiti wa Kati wa Taunton na Kituo cha Kiislamu kilichopo Tower Lane yalivunjwa alfajiri ya Septemba 6.

Mwanaume mwenye umri wa miaka 34 alijisalimisha baadaye na akakamatwa kwa tuhuma za kuharibu mali kwa misingi ya chuki ya kidini au ya kikabila. Polisi bado wanamtafuta mtu wa pili anayehusishwa na tukio hilo.

Sajjad Jabarkhel, mfanyakazi wa msikiti huo, alisema kuwa shambulio hilo limewaathiri waumini kwa kiwango kikubwa. “Kuna hisia za maumivu na kuvunjika moyo kwamba jambo hili limetokea, na lina gharama yake,” aliiambia ITV News.

Aliongeza kuwa waumini wengi wa msikiti huo wanauchukulia Taunton kuwa ni nyumbani kwao, jambo linalofanya kitendo hicho kuwa cha kuumiza zaidi.

Mbunge wa eneo hilo, Gideon Amos, alilaani vikali tukio hilo, akiwataja waliohusika kuwa ni “watu dhaifu na waoga.” Kupitia chapisho la mitandao ya kijamii, alisema kuwa wahusika “hawakaribishwi katika mji wetu” na akaahidi kuwa yeyote atakayeharibu maeneo ya jamii “ataadhibiwa kwa nguvu zote za sheria.”

Polisi wametaja tukio hilo kuwa ni uhalifu wa chuki na wametoa wito kwa yeyote mwenye taarifa, au anayemiliki picha za CCTV, dashcam, au kamera za mlangoni kutoka eneo hilo, awasiliane nao mara moja.

3494574

Habari zinazohusiana
captcha