IQNA

Rais wa Iran alaani ugaidi wa Israel wa kuwalenga viongozi wa Hamas jijini Doha

11:15 - September 10, 2025
Habari ID: 3481211
IQNA-Rais Masoud Pezeshkian wa Iran ameulaani vikali utawala haramu wa Israel kwa kitendo chake 'haramu, cha kinyama na kinacholenga kuvuruga amani ya eneo,' baada ya utawala huo wa Kizayuni kushambulia ardhi ya Qatar na kuwaua shahidi viongozi kadhaa wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas.

Katika taarifa aliyoitoa jana Jumanne, Rais wa Iran amesisitiza kuwa, kitendo cha kigaidi cha kuwalenga viongozi wa Hamas huko Doha kimeweka wazi ukweli kwamba, utawala wa Kizayuni hauna mipaka katika kufanya uhalifu na mauaji, sambamba na kuvuruga juhudi zozote za diplomasia.

Amesisitiza kwamba Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, na taasisi nyingine za kimataifa zinatarajiwa ziteo majibu madhubuti mara moja, kwa uamuzi, na kivitendo, dhidi ya uchokozi huo wa wazi. Amebainisha kuwa, amani ya kudumu katika eneo hili inawezekana tu kwa kukomesha uvamizi na chokochoko za Wazayuni.

Kadhalika Rais Pezeshkian amezitaka nchi za Kiislamu kuwa na msimamo mmoja na wa kivitendo katika kulaani na kukabiliana na jinai za utawala pandikizi wa Israel na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inasimama kidete na ndugu zao wa Qatar katika kukabiliana na uvamizi wa Tel Aviv.

Katika mazungumzo ya simu Jumanne jioni na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, Dakta Pezeshkian amelaani vikali shambulio hilo la Israel dhidi ya Qatar, na kutangaza mshikamano kamili wa Iran na taifa hilo la Ghuba ya Uajemi. "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasimama pamoja na ndugu zao nchini Qatar na itachukua hatua yoyote muhimu ili kumuunga mkono jirani na rafiki yake huyo wa karibu," amebainisha Pezeshkian.

Rais wa Iran ameonya kuwa Israel, kwa kisingizio cha kujilinda, imevuruga amani na usalama wa eneo zima, na wala haionyeshi kusita wala kujali katika kufanya ukatili na jinai katika eneo. Pezeshkian ameongeza kuwa, Israel haiheshimu kanuni za kimataifa au mifumo ya kisheria, akisisitiza kwamba hatua za kijinai za utawala huo zinaendelea kutokana na kuungwa mkono na Marekani.

Kwa upande wake, Sheikh Tamim amempongeza na kumshukuru Rais Pezeshkian kwa kuwasiliana naye na kulinyooshea taifa hilo mkono wa pole na udugu, akielezea wasiwasi wake juu ya ukatili wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu. "Kama ulivyoashiria, mhalifu Netanyahu hana mipaka katika kutenda uhalifu wake. Kwa bahati mbaya, anashambulia na kupiga mabomu popote anapotaka, bila kukumbana na kikwazo chochote," amesema Amir wa Qatar.

4304345

Habari zinazohusiana
captcha