Jumba kubwa zaidi la maonyesho ya mambo ya kale ya Kiislamu ambalo liko katika moja ya viunga vya Cairo, mji mkuu wa Misri litafunguliwa katika wiki chache zijazo baada ya kufanyiwa ukarabati wa miaka saba.
Jumba hilo lilifungwa mwaka 2003 kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati huo na viongozi wa jumba hilo wametangaza kwamba baada ya kufanyiwa ukarabati wa muda mrefu wanatazamia kufunguliwa kwake mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti. Jumba hilo lililojengwa mwanzoni mwa karne ya ishirini lina zaidi ya vitu elfu thalathini vya kale vya Kiislamu yakiwemo mapanga, mazulia na zana za vita. Wasimamizi wa jumba hilo muhimu linalohifadhi athari na mambo ya kale walichukua uamuzi wa kuukarabati kutokana na uharibifu uliofanywa katika baadhi ya sehemu zake na mmomonyoko wa udongo. Akizungumza na waandishi habari, Muhammad Abbas Salim mkuu wa jumba hilo la maonyesho ameashiria kuzeeka kwa baadhi ya sehemu zake na kusema kuwa baadhi ya kuta zake zilikuwa zimepasuka na kupata nyufa kutokana na mmomonyoko wa udongo na hivyo kuhatarisha maisha ya wageni wa jumba hilo pamoja na vitu vya kale vilivyowekwa humo. Amesema kuwa ziadi ya vitu vya kale 1700, vikiwemo vya kipindi cha watawala wa Bani Ummayyia na pia milango ya Msikiti Mkuu wa al-Azhar iliyotengenezwa kwa amri ya khalifa wa Fatimiyun, vitawekwa katika sehemu iliyokarabatiwa ili viweze kutembelewa na wageni.627904