Licha ya hatua ya Kasisi Terry Jones wa kanisa dogo la Dove World Outreach Center katika jimbo la Florida ya kuakhirisha mpango wake wa kutaka kuchoma Qur'ani Tukufu tarehe 11 Septemba, Wakristo wengine walio na misimamo ya kupindukia mpaka nchini Marekani wamechanachana kitabu hicho kitakatifu wakidai kuwa Uislamu unahatarisha usalama wa nchi hiyo.
Kitendo hicho kilichofanyika katika siku ya kumbukumbu ya mashambulio ya Septemba 11 huko Washington kwa mara nyingine tena kinaweka wazi chuki na ubaguzi unaotawala jamii ya Marekani dhidi ya Uislamu.
Kitendo hicho cha dharau dhidi ya Qur'ani Tukufu hakikukomea mjini Washington tu bali kimerejelewa na maadui hao wa Uislamu katika eneo la yaliyokuwa majengo pacha mjini New York na katika kanisa moja huko katika jimbo la Kansas nchini Marekani. Wakristo hao walio na chuki kali dhidi ya Uislamu wamechana kitabu hicho kitakatifu na hivyo kuudhi zaidi ya Waislamu bilioni moja na nusu duniani.
Hii ni katika hali ambayo vyombo vyote vya habari vya kimataifa vilikuwa vimezingatia mpango wa Terry Jones wa kutaka kuichoma Qur'ani. Kasisi huyo anayeongoza kanisa la wafuasi 50 tu katika jimbo la Florida siku ya Ijumaa alilazimika kuakhirisha mpango wake huo kutokana na mashinikizo ya Waislamu ulimwenguni.
Maneno ya kasisi huyo kuwa hatakichoma tena kitabu hicho yanathibitisha wazi dhana ya wengi waliokuwa wakisema kuwa alianzisha wimbi la makelele duniani kwa sababu tu ya kutaka kujipatia umashuhuri. Ni wazi kuwa kitendo hicho cha kuwakera Waislamu zaidi ya bilioni moja kwa kisingizio cha uhuru wa kusema hakiambatani hata kidogo na mantiki iliyo salama. Wamarekani wanapasa kutambua nukta hii muhimu kwamba hakuna jambo lolote linalopasa kuhalalisha dharau dhidi ya matukufu ya watu wengine. 652514