Taarifa ya muungano wa FIOE imeashiria mpango wa kanisa la Marekani wa kuchoma moto Qur’ani na hatua ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ya kumpa zawadi mchora vibonzo aliemvunjia heshima Mtume wa Uislamu wa Denmark na kulaani vikali vitendo hivyo.
Taarifa hiyo imesema kuwa wimbi la kuvunjia heshima matukufu ya dini ya Kiislamu limeongezeka kwa ruhusa ya viongozi na uhamasishaji wa vyombo vya habari na shakhsia wa taasisi za kisiasa na kidini.
Taarifa ya Muungano wa Jumuiya za Kiislamu Barani Ulaya imeongeza kuwa jambo linalotia wasiwasi mkubwa zaidi ni kuwa watekelezaji wa vitendo hivyo viovu wanakaribishwa na viongozi wa ngazi za juu wa nchi za Ulaya.
FIOE imetaka kuchukuliwe hatua madhubuti ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku vitendo vya kuvunjia heshima dini ya Kiislamu, kuwafuatilia na kuwaadhibu watu wanaotekeleza vitendo hivyo. Vilevile imesisitiza juu ya kukomeshwa vitendo hivyo kwa njia ya kutoa mafunzo, vyombo vya habari na harakati za kiutamaduni.
Imesema kuwa ni makosa kudhani kuwa vitendo hivyo vya dharau vitaishia katika kuulenga Uislamu na matukufu yake pekee, bali lengo lake ni kutokomeza thamani za kibinadamu, kutishia misingi ya maadili mema, maisha ya amani na kuheshimiana. 655900