IQNA

Malalamiko ya maulamaa wa Kuwait kuhusu matamshi ya dharau ya kasisi wa Misri dhidi ya Qur'ani

11:54 - September 26, 2010
Habari ID: 2001499
Takwa la kasisi mmoja wa misri la kutaka kufutwa aya moja ya Qur'ani Tukufu anayodai iliongezwa katika kitabu hicho kitakatifu baada ya kuaga dunia Mtume Mtukufu (saw) na katika kipindi cha utawala wa khalifa wa tatu, limeamsha hasira ya wanazuoni na wasomi wa Kuwait ambao wanasema kuwa linatokana na ujahili wake kuhusiana na jinsi aya za Qur'ani zilivyokusanywa na kuandikwa.
Kwa mujibu wa gazeti la Kuwait la ar-Rai, Kasisi al-Anba Bishoy, Katibu wa Jumuiya ya Kikristo ya Misri hivi karibuni alidai katika mkutano mmoja huko Cyprus kwamba kuna aya iliyozidishwa kwenye Qur'ani baada ya kuaga dunia Mtume (saw) na kutaka aya hiyo ifutwe kwa sababu inagongana na itikadi za Kikristo.
Akizungumzia suala hilo Nadhim al-Misbah, Mkuu wa Kamati ya Fatuwa ya Jumuiya ya Kiislamu ya Ihyau at-Turaath ya Kuwait amesema kuwa Waislamu wote wanaamini kwamba Mwenyezi Mungu alikamilisha Qur'ani Tukufu kabla ya kuaga dunia Mtume (saw) na kwamba wahyi ulikatika baada ya kuaga dunia Mtukufu huyo. Wanaamini kwamba jambo alilofanya khalifa wa tatu ni kukusanya pamoja aya zilizokuwa tayari zimeandikwa na kutawanyika sehemu mbalimbali mikononi mwa masahaba.
Katika upande wa pili, Shafi' al-Ajami, mhadhiri wa Masuala ya Kiislamu katika Chuo cha Masuala na Utafiti wa Kiislamu cha Kuwait, katika kumjibu kasisi huyo ametosheka na maneno yafuatayo: 'Si kila neno batili linapasa kujibiwa.'
Naye Suleiman al-Ma'rifi mmoja wa manazuoni mashuhuri wa Kuwait amesema kuwa Qur'ani ni hoja tosha ya Mwenyezi Mungu kwa majini na wanadamu wote wakiwemo Mayahudi, Wakristo na wasiokuwa Waarabu na kwamba maadamu kitabu hicho kitaendelea kulindwa na Mwenyezi Mungu, kama anavyosisitiza Mwenyewe, hakuna mtu yoyote atakayeweza kukipotosha wala kukidhuru hata wakikusanyika pamoja wanadamu na majini wote kwa lengo hilo.
Saad al-Inzi, mwandishi wa Kuwait amesema kuwa shaka na upotoshaji umekuwa ukifanywa na Wakristo na Mayahudi dhidi ya Kitabu hiki kitakatifu tokea wakati wa kudhihiri Uislamu lakini hadi sasa wameshindwa kufikia lengo lao hilo ovu. 661880
captcha