Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC amekaribisha taarifa iliyotolewa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva inayolaani hatua za hivi karibuni za ubaguzi, utumiaji mabavu na chuki dhidi ya dini na kusisitiza juu ya udharura wa kukabiliana na mambo kama hayo.
Katibu Mkuu wa OIC Ekmeleddin Ihsanoglu amesisitiza kuwa kutolewa taarifa hiyo katika kipindi cha sasa ambapo chuki dhidi ya dini kama ubaguzi, kuhusisha ugaidi na dini, kuvunjiwa heshima na kuharibu vitabu vitakatifu na maeneo matukufu ya kidini vimekithiri, kutakuwa na taathira kubwa zaidi.
Vilevile amelipongeza Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwa kuitaka jamii ya kimataifa kukabiliana na utumiaji mabavu na hujuma dhidi ya dini. Ihsanoglu ameashiria pia azimio la Jumuiya ya Nchi za Kiislamu linalopinga vitendo vyote vinavyovunjia heshima matukufu ya dini mbalimbali na kusema kuwa jumuiya hiyo ina nafasi muhimu katika kukabiliana na ubaguzi na chuki za kidini.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ameitaka jamii ya kimataifa kuheshimu taarifa ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kuungana na OIC katika juhudi zake za kupambana na ubaguzi, chuki za kidini na kuimarisha amani na utulivu kote duniani. 668380