IQNA

Kongamano la kimataifa la Mustakbali wa Uislamu Barani Ulaya kufanyika Ubelgiji

11:52 - October 09, 2010
Habari ID: 2008914
Kongamano la kimataifa la Mustakbali wa Uislamu Barani Ulaya litafanyika tarehe 29 hadi 31 Oktoba nchini Ubelgiji.
Kongamano hilo limetayarishwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Ulinganiaji wa Uislamu na Mjumuiko wa Kiislamu wa Ulaya.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sayansi ya Kiislamu cha Ibn Sina nchini Ufaransa Muhammad Bishari amesema kuwa Ubelgiji imeteuliwa kuwa mwenyeji wa kongamano hilo kutokana na kuwa kwake Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya na inatarajiwa kuwa maamuzi yatakayochukuliwa katika kongamano hilo yatakuwa na nafasi muhimu katika maamuzi ya Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kusahilisha hali ya Waislamu barani Ulaya.
Ameongeza kuwa kongamano hilo ni fursa nzuri ya kuchunguza wimbi la chuki dhidi ya Uislamu huko Ulaya na mustakbali wa Waislamu barani humo. Amesema kuwa miongoni mwa malengo ya kongamano hilo ni kudhihirisha tawira sahihi ya Uislamu, kusisitiza juu ya thamani zinazokutanisha pamoja dini mbalimbali na kuarifisha Uislamu kama sehemu muhimu ya utambulisho wa Ulaya.
Muhammad Bishari amesisitzia kuwa malengo mengine ya kongamano hilo ni pamoja na kusisitiza juu ya udharura wa kuishi pamoja kwa amani badala ya kueneza uhasama dhidi ya Uislamu, kueneza moyo wa maelewano kati ya jamii za watu wa Ulaya, kuchunguza mustakbali wa mawasiliano na maelewano kwa ajili ya kufikia hali ya kuishi pamoja kwa amani na kadhalika.
Bishari amesema kuwa kongamano hilo pia litachunguza historia ya Waislamu barani Ulaya, msimamo wa Uislamu kuhusu baadhi ya masuala ya sasa kama demokrasia, wanawake, taswira ya Uislamu katika mifumo ya elimu, taasisi za propaganda na jumuiya za kidini za Magharibi na Uslamu na mazungumzo kati ya dini mbalimbali.
Kongamano hilo linahudhuriwa pia na wawakilishi wa jumuiya za Kiislamu barani Ulaya, Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC na Wizara za Sheria na Mambo ya Ndani za Ubelgiji. 670767

captcha