IQNA

Televisheni ya kwanza ya Kiislamu kwa lugha ya Kitaliano kuzinduliwa

13:25 - October 09, 2010
Habari ID: 2009069
Jamii ya Waislamu walio wachache nchini Italia inapanga kuanzisha hivi karibuni televisheni ya kwanza ya Kiislamu kwa lugha ya Kitaliano.
Kwa mujibu wa televisheni ya al-Jazeera, televisheni hiyo itakuwa ikitangaza habari na matukio yote ya Kiislamu yanayowahusu Waislamu wa nchi hiyo na pia kutangaza shughuli za vituo na taasisi za Kiislamu katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.
Hamza Rocado, msimamizi wa kitengo cha habari na maelezo cha Muungano wa Waislamu Walio Wachache wa Italia amesema kuwa televisheni hiyo ya satalaiti itakuwa na makao makuu yake mjini Roma, mji mkuu wa Italia na kwamba hivi sasa suala linalojadiliwa ni jinsi ya kugharamia shughuli zake pamoja na mishahara ya wafanyakazi.
Amesema, muungano huo umewapelekea barua wakurugenzi na wasimamizi wa vituo mbalimbali vya Kiislamu vya nchi hiyo ukiwataka watoe mapendekezo yao kuhusiana na jinsi ratiba na mipango ya televisheni hiyo inapaswa kutekelezwa.
Rocado ameongeza kwamba kwa kuzingatia kuwa sehemu kubwa ya Waislamu wa Italia ni ya wahajiri ambao hawafahamu vyema lugha ya Kitaliano, muungano huo wa Kiislamu umekusudia kuzingatia zaidi upashaji habari wa picha kuliko mbinu nyinginezo za upashaji habari.
Amesema mwishoni kwamba, televisheni hiyo itakuwa na maripota katika sehemu zote za Italia na kuhojiana na shakhsia mashuhuri wa nchi hiyo. 670528
captcha