IQNA

Bendera ya Haram ya Imam Hussein (AS) Kubadilishwa Jumanne

23:38 - June 15, 2026
Habari ID: 3482364
IQNA – Katika kuukaribisha mwezi wa Muharram wa kalenda ya Hijria, Idara ya Mfawidhi wa Haram Tukufu ya Imam Hussein (AS) mjini Karbala, Iraq, imetangaza tarehe ya hafla ya kubadilisha bendera ya kuba la haram hiyo.

Kwa mujibu wa Jidar Baghdad, idara ya haram hiyo ilieleza kuwa hafla ya kubadilisha bendera ya kuba la kaburi takatifu au Haram ya Imam Hussein (AS) itafanyika Jumanne, tarehe 16 Juni, baada ya Sala ya Magharibi katika uwanja wa haram tukufu.

Hafla ya kubadilisha bendera hiyo huashiria mwanzo wa shughuli na majlisi za kuadhimisha kumbukumbu ya mapambano na kusimama kwa haki kwa Imam Hussein (AS), pamoja na kuwasili kwa mwezi wa Muharram.

Muharram ni mwezi wa kwanza katika kalenda ya Hijria ya Kiislamu.

Waislamu wa madhehebu ya Shia, pamoja na wengine katika maeneo mbalimbali ya dunia, kila mwaka huandaa majlisi na shughuli za maombolezo katika mwezi wa Muharram kuadhimisha kumbukumbu ya kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS) na wenzake.

Imam wa tatu wa Shia (AS), pamoja na kundi dogo la wafuasi wake na baadhi ya wanafamilia wake, waliuawa shahidi na mtawala dhalimu wa zama zake, Yazid bin Muawiya, katika Vita vya Karbala siku ya kumi ya Muharram, maarufu kama Siku ya Ashura, mnamo mwaka 61 Hijria sawa na 680 Miladia.

Mwaka huu, mwezi wa Muharram utaanza Jumanne tarehe 16 Juni, huku Siku ya Ashura ikitarajiwa kuwa tarehe 25 Juni.

3497842

captcha