Kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la IQNA, hayo yamesemwa na Ismail Haniyyah, Waziri Mkuu wa serikali ya Palestina ambaye alikuwa akizungumza katika kikao cha nne cha Baraza Kuu la Muungano wa Idhaa na Televisheni za Kiislamu mjini Tehran kupitia njia ya video conference.
Haniya amesema kuwa hii leo vyombo vya habari vya Wazayuni vinafanya juhudi kubwa za kudhibiti upashaji habari na fikra za mataifa ya Kiarabu na Kiislamu na kusisitiza kwamba, stratejia moja inapasa kutekelezwa kwa madhumuni ya kukabiliana na njama hiyo ya Wazayuni.
Amesema, utekelezwaji wa stratejia hiyo hauna maana ya kubanwa fikra wala mapendeleo tofauti katika sekta ya upashaji habari, bali suala hilo linaweza kuchangia pakubwa katika kunyanyua nafasi ya umoja wa nchi za Kiislamu katika kupambana na propaganda za maadui wa Uislamu. Haniyyah amesema hii leo vyombo vya habari vya Kiislamu vina jukumu zito hasa kuhusiana na kuakisiwa vyema suala la Palestina ulimwenguni.
Amesema, jukumu hilo linaongezeka maradufu kwa kutilia maanani kwamba, kikao cha Baraza Kuu la Muungano wa Redio na Televisheni za Kiislamu kinafanyika mwaka huu katika hali ambayo Ukanda wa Gaza umezingirwa na Wazayuni, ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na Kiyahudi umeimarishwa katika ardhi za Wapalestina na hasa katika eneo takatifu la Quds, vikwazo vya kidhulma vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa vinatekelezwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za kikoloni zinaitishia kijeshi na kiuchumi nchi hii ya Kiislamu.
Waziri Mkuu wa Palestina ameashiria mazungumzo eti ya amani na ahadi zinazotolewa na Marekani kwa Wapalestina na kusema kuwa mazungumzo na ahadi hizo hazina maana yoyote kwa taifa la Palestina.
672204