IQNA

Iran yajibu uchokozi wa Israel, yashambulia kambi za kijeshi

15:08 - June 08, 2026
Habari ID: 3482335
IQNA-Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza kuanzisha “Operesheni Nasr” (Ushindi), likisema limezilenga kambi za kimkakati za anga za utawala wa Israel za Nevatim na Tel Nof, kama hatua ya kujibu mashambulizi ya makombora yaliyolenga vituo vya rada vya Iran.

Vikosi vya ulinzi vya Iran jana usiku viliyatangwa kwa makombora maeneo kadhaa ya Israel, ikiwa ni katika kujibu mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya Lebanon kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano. Kufuatia operesheni hiyo majeshi ya utawala haramu wa Israel yametekeleza hujuma dhidi ya Iran na hivyo kulazimu vikosi vya Iran kutoa jibu kali.

Kwa mujibu wa taarifa ya IRGC iliyotolewa Jumatatu, Kikosi chake cha Anga na Anga za Mbali kilitekeleza operesheni ya kujibu uchokozi wa Israel chini ya kaulimbiu ya kioperesheni “Ya Haidar Karrar”, na heshima ya mashahidi wa vita vya siku 12 vya Juni 2025.

Taarifa hiyo imesema: “Tumetekeleza operesheni hii kujibu uchokozi wa makombora wa utawala wa Kizayuni unaoua watoto, uliolenga vituo kadhaa vya rada katika maeneo matatu nchini Iran."

IRGC imesisitiza kuwa kuwa vitengo vyake vyote vya vita vipo katika hali ya utayari kamili kutekeleza mashambulizi mapana “ya kutoa funzo” katika nyanja zote, huku mipango ya hatua ikiwa imeandaliwa kulingana na mazingira tofauti ya adui.

Taarifa hiyo ilionya kwamba “adui Mzayuni” ameanzisha mchezo hatari kwa kulenga miundombinu ya kiraia na sekta ya mafuta, na kwamba wigo wa majibu utajumuisha malengo yote ya nishati katika eneo zima.

IRGC ilisema pia kuwa “dhima ya madhara ya kiuchumi kwa dunia itabebwa na mchochezi mkuu wa moto katika uwanja huu, yaani Marekani.”

Mashambulizi ya IRGC dhidi ya Kambi ya Anga ya Nevatim kusini mwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel, na Kambi ya Anga ya Tel Nof karibu na Tel Aviv, yalikuja baada ya utawala wa Kizayuni kulenga maeneo ya magharibi na kati mwa Iran Jumatatu asubuhi pamoja na kituo cha petrokemikali kusini mwa nchi.

Vyombo vya habari vya Iran viliripoti kusikika kwa milipuko katika miji ya Tehran, Isfahan na Tabriz kufuatia mashambulizi ya Israel.

Jumapili, IRGC ilirusha makombora ya balistiki kuelekea Kambi ya Anga ya Ramat David kaskazini mwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, ikisema ni jibu kwa kile ilichokitaja kuwa uhalifu mpana wa utawala wa Kizayuni kusini mwa Lebanon, ikiwemo mauaji na kuwahamisha raia.

Akaunti ya mtandaoni ya Shirika la Ujasusi la IRGC ilitangaza Jumatatu kuwa mashambulizi ya kijeshi, kiusalama na ya mtandaoni yaliyofanywa usiku kucha dhidi ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu yalifanikiwa kikamilifu.

Kikosi cha anga cha IRGC pia kimetangaza kulenga maeneo ya viwanda katika mji wa Haifa kwa makombora Jumatatu, kama kulipiza moja kwa moja mashambulizi ya adui dhidi ya sekta ya petrokemikali ya Iran.

Chanzo cha kijeshi chenye ufahamu wa kina, kilichonukuliwa na shirika la habari la Tasnim, kimesema Iran ilitumia mchanganyiko wa makombora ya Emad, Qadr F na Kheibar Shekan ya kizazi cha karibuni katika mashambulizi yake ya Jumatatu dhidi ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. IRGC imesema operesheni zote dhidi ya Israel zimetekelezwa kwa mafanikio makubwa.

IRGC imeonya kuwa ikiwa Israel itaanzisha mashambulizi mengine, wigo wa kijiografia na kijeshi wa operesheni za kujibu za Iran utapanuliwa kwa kiasi kikubwa, na kwamba malengo yote ya Marekani na Israel katika eneo hilo yanaweza kulengwa.

Kamandi ya Khatam al‑Anbiya ya Majeshi ya Iran imetoa taarifa Jumatatu mchana na kusema kwa sasa operesheni za kijeshi dhidi ya Israel zimemalizika lakini imeonya kwamba kuwa Israel itakumbana na mapigo “makubwa na ya kujutia” iwapo itapanua mashambulizi yake kusini mwa Lebanon na hasa katika kitongoji cha kusini cha Beirut cha Dahiyeh.

3497759

captcha