Licha ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran Ayatullah Ali Khamenei kutoa fatuwa hivi karibuni akiharamisha hatua yoyote ya kuwavunjia heshima shakhsia wanaoheshimiwa na Ahlusunna, ambayo ilipongezwa na vyombo vya habari vya kimataifa na wanazuoni wa madhehebu mbalimbali ya Kiislamu, kanali ya televisheni ya al Jazeera ya Qatar ingali inaendeleza stratijia yake ya kutaka kuzusha hitilafu kati ya Waislamu kwa kutayarisha vipindi vinavyowapiga vita Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Televisheni ya al Jazeera inafanya juhudi kupitia vipindi na matangazo yanayoongozwa Mawahabi na kudhaminiwa kwa fedha za Magharibi, za kuzusha mifarakano kati ya Waislamu wa madhehebu za Shia na Suni kwa kualika viongozi mashuhuri wenye misimamo mikali ya Kiwahabi katika vipindi vyake.
Hivi karibuni televisheni hiyo ilimwalika Muwahabi mashuhuri Muhammad al Arrifi kutoka Saudi Arabia na Othman al Khamis mmiliki wa kanali ya televisheni iliyosimamishwa katika satalaiti ya Nailsat ya al Safa kutokana na vipindi vyake vinavyochoea hitilafu na mifarakano kati ya Waislamu. Katika kipindi hicho al Arrifi alitoa visa vya orongo dhidi ya madhehebu ya Shia huku mgeni mwenzake katika kipindi hicho Othman al Khamis akiwasifu na kuwapongeza Bani Umayya hususan Muawiya bin Abu Sufiyan na Yazid bin Muawiya na Abu Sufiyan mwenyewe.
Kipindi hicho kilishambulia wafuasi wa madhehebu ya Shia na itikadi zao na kuwazulia urongo Maimamu watoharifu katika kizazi cha Bwana Mtume Muhammad (saw). La kustaajabisha ni kuwa watayarishaji wa kipindi hicho hawakuwaalika wanazuoni wa madhehebu ya Shia kujibu tuhuma na orongo wa Mawahabi hao.
Kipindi hicho cha televisheni ya al Jazeera ya Qatar kimechochea zaidi tabia ya kuwakufurisha Waislamu wa madhehebu ya Shia, kuwavunjia heshima Maimamu watoharifu katika kizazi cha Mtume Muhammad (saw) na fitina za kimadhehebu kati ya Waislamu.
Kipindi hicho kimerushwa hewani siku chache tu baada ya Ayatullah Ali Khamenei kutoa fatuwa akiharamisha kuwavunjia heshima wake za Mtume (saw). Vilevile Sheikh wa al Azhar Ahmad al Tayyib alitoa taarifa akipinga fatuwa za Mawahabi za kuwakufurisha Waislamu wa madhehebu ya Shia na kusema kuwa Masuni wanasali jamaa nyuma ya ndugu zao Mashia. 682901