IQNA

Kasisi wa Misri awapa zawadi mahafidhi wa Qur'ani Tukufu

11:47 - October 27, 2010
Habari ID: 2020676
Kasisi mmoja wa Misri katika mji wa Mansura amewazawadia mahafidhi kadhaa vijana wa Qur'ani kitabu hicho kitakatifu pamoja na zawadi nono ya fedha.
Kwa mujibu wa gazeti la nchi hiyo la al-Yaum as-Sabe', Rumani Farid Kasisi wa Kikopti aliwatunukia mahafidhi hao zawadi hiyo ya Qur'ani ikiandamana na fedha nono katika hafla hiyo aliyofanyika kwa ubunifu wake.
Idadi kubwa ya shakhsia wa Kiislamu na wawakilishi wa Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Misri walishiriki katika hafla hiyo iliyofanyika hapo jana Jumanne.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rumani Farid amesema kuwa mivutano na ghasia zilizojiri huko nyuma kati ya Waislamu na Wakristo wa Misri zilitokana moja kwa moja na masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii na kwamba hakuna wakati ambapo wafausia wa dini mbili hizo walizozana kwa sababu za kidini.
Ameelezea masikitiko yake makubwa kutokana na kitendo cha baadhi ya makasisi wenye misimamo ya kupindukia mipaka nchini Marekani cha kuchoma moto Qur'ani na kwamba Wakristo wa Misri walifanya maandamano kulaani kitendo hicho cha jinai.
Kasisi Rumani Farid amesema dini zote za mbinguni zinasisitiza juu ya kuzingatiwa misimamo ya wastani na kujiepusha na tabia za utumiaji mabavu, kuondoa fitina na kuishi pamoja kwa amani na urafiki wafuasia wa dini tofauti katika jamii. 683180
captcha