IQNA

Kikao cha kumuadhimisha Ali Asghar (as) kufanyika Saudi Arabia

19:00 - December 08, 2010
Habari ID: 2044806
Kikao cha kimataifa cha kumuadhimisha Hadhrat Ali Asghar (as) kimepangwa kufanyika siku ya Ijumaa tarehe 10 Disemba nchini Saudi Arabia. Kikao hicho kitafanyika katika Husseiniya ya Zeinabiyya katika mji wa Awamiya katika mkoa wa Qatif.
Husseiniya hiyo imetangaza kuwa kikao hicho kitaanza saa moja na nusu asubuhi na kwamba akina mama walio na watoto wachanga wanaonyonya wataruhusiwa kushiriki katika kikao hicho. Tangazo la Husseiniyya hiyo limesema kwamba itashirikiana na Jumuiya ya Kimataifa ya Hadhrat Ali Asghar (as) kwa lengo la kuhuisha marasimu ya watoto wachanga wanaonyonya wa Imam Hussein (as) ili kukumbuka tukio chungu la kuuawa shahidi Ali Ashgar, mtoto mchanga aliyekuwa na umri wa miezi sita wa Imam Hussein (as) katika ardhi ya Karbala. Lengo hasa la kuhuishwa marasimu hiyo ni kubainisha nara za Imam Hussein (as) pamoja na thamani za harakati yake, kufikisha ujumbe wa kudhulumiwa Imam Hussein na mtoto wake mchanga Hadhrat Ali Asghar (as) kwa walimwengu, kuwafahamisha walimwengu tukio chungu la Ashura na ujumbe wake ambao ni wa kurekebisha umma wa Kiislamu, kuamrisha mema na kukataza mabaya, kupambana na dhulma na madhalimu na hatimaye kuthibitisha ukhalifa na uimamu wa maimamu watoharifu (as).
Jumuiya ya Kimataifa ya Hadhrat Ali Asghar (as) ni jumuiya isiyo ya kiserikali ambayo kila mwaka hufanya vikao maalumu vya kumuadhimisha Hadhrat Ali Asghar (as) katika nchi mbalimbali za Kiislamu ikiwemo Iran. 708568
captcha