IQNA

Shia na Suni wa Saudia watia saini hati ya mapatano

16:55 - December 26, 2010
Habari ID: 2053639
Shakhsia wakubwa wa Kishia na Kisuni wa Saudi Arabia wametia saini hati ya suluhu katika mji mtakatifu wa Madina.
Hati hiyo ya suluhu ilitiwa saini jana Jumamosi kwa anwani ya 'kuishi pamoja kwa amani kama watu wa familia moja'. Hati hiyo imetiwa saini kufuatia matukio ya siku ya Ashura mwaka huu mjini Madina.
Sherehe ya kutiwa saini hati hiyo ambayo ni ya kwanza ya aina yake imehudhuriwa na shakhsia 200 wa Kishia na Kisuni na maafisa wa serikali ya Saudi Arabia mjini Madina.
Hati hiyo ya suluhu imetiwa saini na Tahir Abdulmun'im al Hajuj na Saleh al Jad'an kutoka madhehebu ya Shia na Faisal Abu Rabia na Sulaiman bin Ghamit al Sa'idi wa madhehebu ya Suni.
Hati hiyo inasisitiza juu ya udharura wa kuishi kwa amani na urafiki kati ya Waislamu wa Shia na Suni, usawa kwa wote, ushirikiano kwa ajili ya kutoa huduma kwa raia wote, kupinga vitendo vya kuvunjiana heshima na kuhamasisha amani katika jamii.
Kikao cha suluhu kati ya maulamaa wa Shia na Suni wa Saudi Arabia kilifanyika Jumatano iliyopita kikisimamiwa na Amir wa eneo la Madina Abdul Aziz bin Majid.
Shughuli za maombolezo ya kuuawa mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein (as) katika siku ya Ashura ya mwaka huu zilivamiwa na Mawahabi wenye misimamo mikali ambao waliwashambulia Waislamu wa madhehebu ya Shia waliokuwa katika maombolezo na kuzusha ghasia na machafuko yaliyopelekea kuharibiwa mali ya umma. 718377
captcha