Akizungumza hivi karibuni na Hamid Muhammad Ali, Balozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC nchini Iraq, Ayatullah Bashir Najafi, mmoja wa mamarja mashuhuri wa nchi hiyo amesema kuwa mji mtakatifu wa Najaf umekuwa na utaendelea kuwa kituo cha kueneza amani na kulindwa damu ya watu.
Ayatullah Najafi amesisitiza juu ya udharura wa kuenezwa utamaduni wa kusameheana na kuvumiliana Waislamu na kujiepusha wafuasi wa madhehebu tofauti za Kiislamu na vitendo vya kutumia mabavu na ghasia. Pia amewataka kujiepusha kukufurishana, jambo ambalo amesema lina madhara makubwa kwa umma wa Kiislamu.
Ayatullah Najafi amebainisha masikitiko yake makubwa kutokana na kuenea hitilafu miongoni mwa Waislamu na vilevile dharau inayoonyeshwa na Wazayuni kwa Waislamu wapatao bilioni moja na nusu duniani. Amesisitiza juu ya udharura wa kuenezwa utamaduni wa kusameheana na kuheshimiana Waislamu wote ulimwenguni. Amelaani fatuwa zinazotolewa na baadhi ya watu wasiofahamu vyema Uislamu na kusisitiza kwamba Waislamu wote watajibu maswali mbele ya Mwenyezi Mungu kuhusiana na kutowajibika kwao katika kuimarisha umoja kwenye umma na kupambana na maadui wa Uislamu.
Ameutaka Jumuiya ya Nchi za Kiislamu kuanzisha mashirika ya habari na vyombo vya mawasiliano ya umma kwa ajili ya kueneza umoja miongoni mwa Waislamu na kuwafikishia walimwengu ujumbe sahihi wa mafundisho ya Kiislamu.
Kwa upande wake, Hamid Muhammad Ali, Balozi wa OIC nchini Iraq amemfikishia Ayatullah Najafi, salamu za Ekmeleddin Ihsanoghlu, Katibu Mkuu wa OIC na kumbainishia mipango ya jumuiya hiyo ya Kiislamu katika kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu wa Iraq na nchi nyingine za Kiislamu. 719215