IQNA

Vijana wa Kishia Afrika Kusini wakutana

13:09 - January 03, 2011
Habari ID: 2057511
Vijana wa madhehebu ya Kiislamu ya Kishia nchini Afrika Kusini wamekutana Januari Mosi katika mkoa wa Mpumalanga.
Mwambata wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Afrika Kusini alitoa hotuba katika mkutano huo wa siku tano uliofanyika katika eneo la Kande Vale mkoani humo.
Akiashiria ujumbe wa hija wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1431 H, Bw.Ahmadi mwambata wa utamaduni wa Iran ametaja majukumu ya vijana kuhusu harakati za Kiislamu duniani ambazo chimbuko lake ni Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Ametoa wito kwa vijana kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Afisa huyo wa utamaduni kutoka Iran amesema vijana wana uwezo mkubwa ambao hawajatumia na amewataka kudumisha heshima na maadili ya kibinadamu huku wakijaribu kunyanyua juu kiwango chao cha elimu.
Baada ya hotuba yake Bw. Ahmadi ametoa zawadi za Qur'ani Tukufu kwa vijana walioshiriki katika hafla hiyo. Zawadi hizo zilijumuisha tafsiri ya Kiingereza ya suratu Yasin, majina ya Mwenyezi Mungu na tafsiri ya Kiingereza, majina ya Ahlul Bayt AS na kitabu cha Familia Katika Uislamu kwa lugha ya Kiingereza kilichoandikwa na Ayatullah Ibrahim Amini.
Mkutano huo pia ulijumuisha kozi ya elimu na masuala ya dini iliyofanyika kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu ya kidini na kiutamaduni ya vijana wa Kishia.
Kati ya yaliyofunza katika kozi hiyo ni masuala ya kisiasa na kijamii ambayo Waislamu wa madhehebu ya Shia wanapaswa kufahamu katika dunia ya leo.
722137
captcha