Kufuatia tukio la kigaidi la hivi karibuni huko Alexandria nchini Misri, Cardinal Jean-Louis Tauran, Mkuu wa Baraza la Mazungumzo ya Kidini la Vatican amezungumzia udharura wa kufuatiliwa kwa makini mazungumzo kati ya Uislamu na Ukristo ili kujenga hali ya utulivu na maelewano kati ya wafuasi wa dini mbili hizi.
Akilaani shambulio hilo kupitia mazungumzo yake na Redio Vatican, Tauran amesema kufuatia tukio hilo kuwa kuna haja kubwa ya kufanyika mazungumzo hayo kuliko wakati mwingine wowote. Amesema katika sehemu nyingine ya mazungumzo hayo kwamba hakuna kipindi kingine cha historia ambapo haja ya kufanyika mazungumzo kati ya Uislamu na Ukristo imehisika kama inavyohisika sasa. Kwa msingi huo amesema viongozi wa kidini wanapasa kulipa umuhimu maalumu suala hilo na kuandaa uwanja wa kukutana pande mbili hizi kwenye meza ya mazungumzo.
Tunaashiria hapa kwamba viongozi wa Kiislamu na Kikristo katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakitoa taarifa za kulaani vikali kitendo hicho cha ugaidi kilichotekelezwa karibu na kanisa la Makopti wa Misri la al-Qiddissin huko katika mji wa Alexandria, wakati waumini wa kanisa hilo walipokuwa wamekusanyika kusherehekea Sikukuu ya Krismasi. 724046