Harakati za kupigania uhuru na kujitawala za wananchi wa Misri na Tunisia zinabainisha wazi kwamba mataifa ya Kiislamu hadi leo yangali yana hisia za uhuru, na kwamba mapambano yanayofanywa na wananchi hao dhidi ya tawala zao dhalimu ni hatua moja muhimu kuelekea kwenye umoja katika ulimwengu wa Kiislamu.
Hayo yamesemwa na Abduraheem Ali mwandishi na mtafiti mashuhuri wa Kiislamu wa nchini Sudan ambaye anahudhuria kikao cha Wiki ya Umoja wa Kiislamu mjini Tehran. Amesema mwamko huo mpya umebadili kabisa historia na kwamba iwapo utadumishwa utaziondoa nchi za Kiislamu katika utegemezi wa nchi za kibeberu na kikoloni za Magharibi.
Amesema ana imani kwamba harakati na mwamko huo utaleta umoja na mshikamano kati ya mataifa ya Kiislamu dhidi ya maadui. Amesema kwa masikitiko makubwa kwamba watawala wa nchi za Kiislamu wamegeuka na kuwa chanzo kikuu cha mgawanyiko na hitilafu miongoni mwa Waislamu. Mtafiti huyo wa Sudan amesema kwamba mapambano dhidi ya dhulma na ufisadi ni matunda ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kwamba madola ya Magharibi yalihofia kuzagaa kwa athari za mapinduzi hayo katika nchi nyingine za Kiislamu na ndio maana zikaweka na kuimarisha watawala dhalimu na vibaraka katika nchi nyingi za Kiislamu, watawala ambao wamekuwa na nafasi muhimu katika kuzusha na kuzidisha hitilafu katika umma wa Kiislamu. 750550