Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo Jumatatu, Machi 21, 2011, alipohutubia makumi ya maelfu ya wafanyaziara katika Haram Tukufu ya Imam Ridha AS mjini Mashhad, kaskazini mashariki mwa Iran, sambamba na siku ya kwanza ya mwaka 1390 Hijria Shamsia. Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) na watu kuenea katika kumbi nyingine za Haram hiyo tukufu. Sambamba na kutathmini harakati jumla ya Iran katika mwaka uliopita wa Kiirani wa 1389 Hijria Shamsia, hususan katika suala la kufanikishwa kaulimbiu ya mwaka huo ya "hima kubwa zaidi na kazi kubwa zaidi" katika nyuga tofauti zikiwezo za sayansi na teknolojia, kuanza utekelezaji wa mpango wa kutoa ruzuku kiuadilifu na kukabiliana na vikwazo vya nchi za Magharibi kwa busara na kwa nguvu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha pia umuhimu wa kaulimbiu ya mwaka huu wa 1390 Hijria Shamsia yaani "mwaka wa jihadi ya kiuchumi"na masuala yanayopaswa kufanywa katika mwaka huu. Aidha ametangaza msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na harakati za hivi sasa za wananchi wa nchi za eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika sambamba na njama zinazofanywa na Marekani na nchi za Magharibi kukabiliana na harakati hizo za wananchi.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei kwa mara nyingine ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa kuingia mwaka mpya wa Kiirani na kuanza sikukuu za Nairuzi kwa taifa la Iran na mataifa yote yanayosherehekea sikukuu hiyo. Vile vile ametathmini kiujumla harakati ya taifa la Iran katika mwaka uliopita wa 1389 Hijria Shamsia na hususan katika upande wa kufanikisha kaulimbiu ya mwaka huo ya "hima kubwa zaidi na kazi kubwa zaidi"na koongeza kuwa, kwa hakika wananchi na viongozi wa Iran mwaka huo walifanya kazi kwa hima kubwa zaidi na kwamba matunda ya jambo hilo yataweza kuonekana zaidi katika siku zijazo. Amesema pamoja na hayo lakini tayari athari nzuri za jitihada hizo zimeonekana katika miezi hii michache katika sekta mbali mbali nchini.
Amesema medani ya sayansi na teknolojia ni moja ya mifano ya wazi ya kufanikishwa kaulimbiu ya "hima kubwa zaidi na kazi kubwa zaidi" na kuongeza kuwa, harakati kubwa ya kielimu ambayo imeanza miaka michache iliyopita nchini Iran hivi sasa imeingia kasi zaidi na kwamba harakati hiyo kubwa ya kielimu inafanyika kwa lengo la kupata utaalamu na teknolojia mpya na bora zinazochipua kila leo duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitaja kazi zinazofanyika katika masuala kama ya teknolojia ya masuala ya maumbile, anga, anga za juu, teknolojia ya Nano, seli shina, kuzalisha dawa kama za kutibu kensa, kuzalisha injini mbali mbali za kisasa, kufanikiwa kutengeneza kompyuta kubwa za kisasa "super computer" kuwa ni miongoni mwa kazi zilizotokana na elimu na teknolojia mpya na bora duniani. Amesisitiza kuwa, wataalamu vijana wa Kiirani wanazidi kusonga mbele kwa kasi katika masuala hayo na kwamba kwa mujibu wa ripoti ya vituo vyenye itibari vya kimataifa, kasi ya harakati ya kielimu nchini Iran imepindukia wastani wa kimataifa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, kuwepo wasomi vijana wenye wastani wa umri wa miaka 35, kuwepo moyo mkubwa wa kujiamini na kuundika mchakato wa kuuza uzalishaji wa elimu na kuzalisha utajiri wa taifa ni miongoni mwa harakati hizo za kielimu. Ameongeza kuwa, kama mchakato wa kuzalisha maarifa, kubadilisha maarifa hayo kuwa teknolojia, kuzalisha bidhaa na hatimaye kufanya biashara ya kielimu kutafanikishwa vizuri, basi bila ya shaka yoyote kutamalizikia kwenye kuzalisha utajiri kitaifa na kukidhi mahitaji wa nchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema kuwa, kuanza kutekelezwa mpango wa kutoa ruzuku kiuadilifu nchini ni miongoni mwa mifano ya kufanikishwa kaulimbiu ya "hima kubwa zaidi na kazi kubwa zaidi" na kuongeza kuwa, kuanza kutekelezwa mpango huo - jambo ambalo linakubaliwa kwa kauli moja na wataalamu wote wa kiuchumi nchini - ilikuwa ni moja ya matumaini ya miaka mingi nchini ambapo kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu hatimaye utekelezaji wa mpango huo umeanza mwaka 1389 (Hijria Shamsia) na ushirikiano wa wananchi na serikali ni mzuri sana katika jambo hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, athari nzuri na za muda mrefu za utekelezaji wa mpango huo zitaonekana katika siku za usoni na kukumbusha kuwa: hata katika kipindi hiki kifupi cha tangu kuanza kutekelezwa mpango huo, matunda yake mazuri yameanza kuonekana.
Amesema moja ya malengo ya mpango wa kutoa ruzuku kiuadilifu ni kugawa kwa uadilifu ruzuku za serikali kwa wananchi kwa ajili ya kufanikisha uadilifu wa kijamii. Ameongeza kuwa, malengo mengine ya mpango huo ni kusimamia vizuri matumizi ya nishati, kuleta marekebisho ya kweli ya kigezo cha matumizi na marekebisho mengine muhimu na yanayotakiwa ya kiuchumi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuongezeka bidhaa zisizo za mafuta zinazosafirishwa nje na kujongea zaidi kwenye lengo kuu la kuacha bajeti ya Iran kutegemea mafuta, kuwa ni mfano mwingine wa kufanikishwa kaulimbiu ya "hima kubwa zaidi na kazi kubwa zaidi" ya mwaka uliopita wa 1389 (Hirjia Shamsia) na kukumbusha kuwa, mfano mwingine wa kufanikishwa kaulimbiui hiyo ni muamala wa busara na makini wa wananchi na viongozi nchini mbele ya vikwazo vya nchi za Magharibi zinazoongozwa na Marekani ambapo kwa bahati nzuri adui amelazimika kutupa silaha zake kutokana na juhudi na kazi za usiku na mchana za viongozi nchini katika sekta tofauti. Amesema maadui hivi sasa wamesalimu amri kiasi kwamba Wamagharibi wenyewe wanakiri kuwa vikwazo havina tena athari kwa Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ametaja hatua zilizochukuliwa katika uzalishaji wa fursa za kazi, ujenzi wa nyumba, miji na vijiji, utengenezaji wa mabarabara na njia za mawasiliano ya elektroniki kuwa ni mifano mingine ya kufanikishwa kaulimbiu ya "hima kubwa zaidi na kazi kubwa zaidi" katika upande wa kiuchumi.
Amesisitiza kuwa, mwaka uliopita wa 1389 (Hijria Shamsia) ulikuwa ni mwaka wa "hima kubwa zaidi na kazi kubwa zaidi" kwa maana halisi ya neno ambapo tab'an suala hilo halihusiana na mwaka 89 tu, kwani mwaka huu na miaka ijayo nayo inabidi liendelee hadi taifa la Iran litakapoweza kufikia kwenye nafasi yake linayostahiki.
Sehemu ya pili ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameifanya maalumu kwa ajili ya kubainisha na kutoa ufafanuzi kuhusiana na sababu za kuitwa mwaka huu wa 1390 (Hijria Shamsia) kuwa mwaka wa "Jihadi ya Kiuchumi."
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, sababu zilizopelekea mwaka 1390 kuitwa mwaka wa "Jihadi ya Kiuchumi" ni kwamba, licha ya kuwa nchini Iran kuna kazi nyingi za kimsingi na za dharura zinazopaswa kufanywa lakini wataalamu wanaamini kuwa moja ya masuala ambayo ni ya dharura zaidi na ni muhimu zaidi hivi sasa ni masuala ya kiuchumi na kufanya kazi kijihadi katika medani hiyo kwani kama Jamhuri ya Kiislamu itaionyesha dunia na walimwengu uwezo wake wa kutatua masuala ya kiuchumi, basi suala hilo litalisaidia sana taifa la Iran kulinda heshima yake na litakuwa na taathira nyingi nzuri.
Amesema moja ya vigezo vikuu vya kupiga hatua za kiuchumi ni kukuwa uchumi kwa mujibu ya ulivyotabiriwa katika "Mpango wa Tano wa Maendeleo." Amefafanua zaidi akisema, katika Mpango wa Tano wa Maendeleo, wastani wa chini wa ukuaji wa uchumi umetabiriwa kuwa asilimia 8 na amewataka viongozi nchini kutumia fursa zote za kukuza uchumi kwa ajili ya kuwaletea maisha bora wananchi kama vile kupunguza kiwango cha ukosefu wa kazi, kuongeza fursa za kazi, kuongeza kiwango cha uwekezaji katika sekta binafsi na kuiwezesha sekta binafsi kupitia kuanzisha asasi mbali mbali za ushirika, kuandaa miundo mbinu inayotakiwa ya kisheria, kuunga mkono ustawi wa kazi, kuandaa mazingira yanayofaa kwa ajili ya kuepusha israfu katika huduma za kimsingi kama vile maji na kushirikishwa moja kwa moja wananchi katika masuala ya kiuchumi.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, kutekeleza mpango wa "Jihadi ya Kiuchumi" kunahitajia kuwepo moyo wa jihadi, kuwa makini kimaanawi na kuheshimiwa masuala ya dini katika jamii hususan kati ya vijana, kujiepusha na masuala ya pembeni-pembeni yasiyo na maana na kulinda mshikamano na umoja kitaifa yaani kati ya wananchi kwa wananchi, kati ya wananchi na viongozi na kati ya viongozi kwa viongozi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema pia kuwa, pamoja na kutajwa mwaka 1390 kuwa mwaka wa "Jihadi ya Kiuchumi" lakini viongozi nchini hawapaswi kufumbia macho masuala mengine hasa katika upande wa sayansi na teknolojia.
Baada ya hapo, Ayatullah Udhma Khamenei ameingia katika sehemu ya tatu ya hotuba yake ambayo ilikuwa ni mahsusi kwa ajili ya kuchambua na kuzungumzia matukio yanayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika na harakati za wananchi katika nchi za Tunisia, Misri, Bahrain, Yemen na Libya.
Amesema kuwa harakati hizo ni muhimu sana na zinaonyesha kwamba kuna mabadiliko makubwa na ya kimsingi yanatokea katika eneo la Kiarabu na Kiislamu kutokana na kuongezeka mwamko wa umma wa Kiislamu. Amekumbusha kuwa, harakati hizo zina sifa mbili kuu, moja ni kushiriki vilivyo wananchi katika medani na pili ni muelekeo wa kidini wa harakati hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja sababu kuu ya harakati zinazoshuhudiwa hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika kuwa ni kujeruhiwa ghera na hisia za heshima na kulinda hadhi za wananchi wa eneo kutokana na vitendo visivyo sahihi vya watawala wao madhalimu. Ametoa mfano akisema kuwa, kwa mfano vitendo vya Husni Mubarak nchini Misri na hatua yake ya kufanya jinai mbaya zaidi kwa niaba ya utawala wa Kizayuni hususan katika kadhia ya Ghaza na vile vile vitendo vya Muammar Gaddafi wa Libya ikiwa ni pamoja na hatua yake ya kuipa Marekani suhula na uwezo wake wote wa nyuklia baada ya kutishwa-tishwa kidogo tu na Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi, ni miongoni mwa vitendo ambavyo vimejeruhi ghera na heshima ya wananchi wa nchi hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amesema, vitisho na mashinikizo ya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani yamekuwepo pia dhidi ya Iran na hadi hivi sasa yapo lakini viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu si tu hawajawahi kulegeza kamba mbele ya vitisho hivyo, lakini pia wanazidi kuongeza uwezo wao wa teknolojia ya nyuklia kadiri siku zinavyosonga mbele.
Aidha amezungumzia miamala ya Marekani mbele ya matukio yanayoendelea katika eneo akisema kuwa, kwanza Wamarekani walionyesha wazi kuwa wameemewa mbele ya matukio hayo na walishindwa kusema chochote na ndio maana walichukua misimamo inayokinzana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kuwaunga mkono madikteta ndiyo misimamo thabiti ya Wamarekani na ndivyo walivyofanya kuhusu Husni Mubarak wa Misri waliyemuunga mkono kwa nguvu zao zote, lakini walipoona kwamba haiwezekani tena kubakia madarakani Mubarak, wamemtupa mithili ya karatasi ya chooni. Amesema inabidi jambo hilo liwe funzo kwa viongozi wengine ambao ni vibaraka wa Marekani.
Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kuangua dikteta wa Misri kuwa ni pigo kubwa kwa siasa za Mashariki ya Kati za Marekani na kuongeza kuwa, wakati Marekani ilipokata tamaa na kuona haiwezi kuwalinda Ben Ali na Husni Mubarak, ilianza kufanya jinai japo kwa kiwango cha chini ili kulinda miundo ya tawala za kidikteta huko Tunisia na Misri lakini hila hizo nazo zilizishindwa na mapinduzi ya wananchi.
Amekumbusha kuwa, baada ya kushindwa katika hila zake za huko nyuma, Marekani ilikuja na njama mpya za kutaka kutumia vibaya fursa iliyojitokeza na kuyateka nyara mapinduzi ya wananchi, lakini njama hizo nazo zimeshindwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia juu ya juhudi za Marekani za kujaribu kupotosha mapinduzi ya wananchi na kutaka kuonyesha kuwa Iran nayo hivi sasa imekumbwa na wimbi kama hilo na kuongeza kuwa, Wamarekani walitumia vitimbakwiri vyao na watu walio na maradhi ya nafsi kutaka kueneza chokochoko zao nchini Iran lakini wananchi wa Iran wako macho na wamezivunjilia mbali njama hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei amevitaja vitendo vya Marekani mbele ya harakati za wananchi katika eneo na madai ya Washington ya kulinda wananchi hao kuwa ni ya kinafiki na huku akiashiria matamshi ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani kuhusiana na kuwaunga mkono wananchi wa Iran amesema: "Sisi hatujui je, Rais wa hivi sasa wa Marekani anajua anachokisema au la, amechanganyikiwa? Anasema, wananchi waliokusanyika katika medani ya Azadi ya Tehran (malengo yao) ni sawa na (ya) wale wananchi wa Misri (waliokusanyika) kwenye medani ya Tahrir (mjini Cairo) wakati ambapo kila mwaka inapofika tarehe 22 Bahaman (Februari 11, zinapofikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran) wananchi hukusanyika kwenye medani ya Azadi mjini Tehran wakiwa na na kaulimbiu yao kuu (yaani mauti kwa Marekani).
Amesisitiza kuwa, madai ya Wamarekani kwamba wanayaunga mkono mataifa mengine duniani siku zote ni uongo kwani si tu Wamarekani hawana huruma na mataifa ya eneo lakini hawana huruma pia kwa wananchi wao wenyewe kwani Rais wa hivi sasa wa Marekani licha ya nchi hiyo kukabiliwa na hali mbaya sana ya kiuchumi, lakini anamimina mabilioni ya dola za wananchi wa Marekani kwenye mapolo ya kampuni za kutengeneza silaha na kufyonza mafuta.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kujadili harakati zinazoendelea hivi sasa za wananchi wa eneo hili kwa kuashiria masuala ya Libya na kusema kuwa, katika masuala ya Libya, Jamhuri ya Kiislamu inalaani mauaji yanayofanywa na serikali dhidi ya wananchi na vile vile inalaani mia kwa mia mashambulizi ya Marekani na nchi za Magharibi dhidi ya nchi hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, madai ya Marekani na nchi za Magharibi ya kwamba mashambulizi yao ya kijeshi yanakusudia kuwalinda wananchi wa Libya hayakubaliki hata kidogo na amehoji akisema, kama kweli madola hayo yako pamoja na wananchi wa Libya kwa nini yalikaa mwezi mzima yakiangalia kwa macho tu jinsi utawala wa nchi hiyo unavyowaua raia hao bila ya kuchukua hatua zozote za kuwalinda wananchi hao.
Amesisitiza kuwa, kinachofuatiliwa na Marekani na nchi za Magharibi huko Libya ni mafuta tu ya taifa hilo na kuweka kambi katika nchi hiyo ili kuja kuzidhibiti tawala (huru za wananchi) zitakazoundwa Tunisia na Misri.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema, hatua zilizochukuliwa na Umoja wa Mataifa kuhusiana na masuala ya Libya ni aibu kwa chombo hicho cha kimataifa na ameongeza kuwa, badala ya Umoja wa Mataifa kuyatumikia mataifa ya dunia umegeuka na kuwa wenzo wa kufanikishia malengo ya Marekani na nchi za Magharibi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea kujadili harakati za wananchi Waislamu wa Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika akisema kuwa, muundo wa harakati ya wananchi wa Bahrain hauna tofauti yoyote na muundo wa harakati za wananchi wa Misri, Tunisia, Libya na Yemen kwani wananchi wa Bahrain nao wanataka wapate haki yao ya kuchagua viongozi wanaowapenda na wala hayo si maombi makubwa.
Hata hivyo amesema, ni Marekani na nchi za Magharibi ndizo zinazozusha suala
la Usuni na Ushia katika masuala ya Bahrain ili madola hayo ya kibeberu yapate upenyo wa kuingilia masuala ya eneo. Ameongeza kuwa, lengo la Marekani la kuzusha suala la Usuni na Ushia katika kadhia ya Bahrain ni kuzuia wananchi wasiunge mkono wala kusaidia harakati ya wananchi huko Bahrain.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameelezea kusikitishwa kwake na baadhi ya watu waliotumbukia kwenye mtego huo wa Marekani na kusisitiza kuwa, kuzushwa suala la Ushia na Usuni katika masuala ya Bahrain kunatoa msaada mkubwa sana kwa Marekani na kwa maadui wa umma wa Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria juu ya uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa taifa la Palestina hasa wakati wa mashambulizi ya siku 22 ya Wazayuni dhidi ya wananchi wa Ukanda wa Ghaza na kukumbusha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa wakati wote ikiliunga mkono taifa Palestina na imeziunga mkono pia harakati za hivi karibuni za wananchi Waislamu wa Tunisia, Misri, Libya na Yemen katika hali ambayo wananchi hao si Mashia kwani Tehran inajua kwamba lililo muhimu hapa ni Uislamu na wala si masuala ya kimadhehebu hivyo linapofika suala la Bahrain pia inabidi hali iwe hivyo hivyo na isiwe ni kunyamazia kimya dhulma wanayofanyiwa wananchi hao kwa kuogopa sumu za maadui wanaozusha suala la Usuni na Ushia katika kadhia hiyo.
Ameashiria pia hatua ya Saudi Arabia ya kuingilia kijeshi mgogoro wa Bahrain na kuongeza kuwa, jeuri na ujuba wa Marekani na vikaragosi wake umechupa mipaka katika eneo kiasi kwamba hatua ya kupelekwa vifaru vya kijeshi vya Saudia huko Bahrain haisemwi kwamba ni uingiliaji wa mambo ya ndani ya nchi hiyo lakini hatua ya Marajii, maulamaa na watu wanaopigania haki ya kulalamikia mauji ya watu huko Bahrain inadaiwa ni uingiliaji wa Iran katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba hatua ya Saudi Arabia ya kuingia kijeshi nchini Bahrain ni kosa na amesisitiza kwamba, hatua hiyo itawafanya wananchi wa eneo waichukie Saudia na bila ya shaka jambo hilo litakuwa na hasara kubwa kwa Saudi Arabia.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, harakati mpya iliyoanza katika eneo ni harakati ya umma wa Kiislamu inayoelekea upande wa kufanikisha malengo ya Uislamu hivyo kama alivyoahidi Mwenyezi Mungu, harakati yenye sifa hizo itashinda tu na silisila za kuzidi kushindwa Marekani katika eneo itazidi kushuhudiwa.
Amesisitiza kukwa, msimamo wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kuhusu masuala yanayoendelea katika eneo ni kulinda wananchi na kuunga mkono haki zao sambamba na kupinga madikteta na wakandamizaji.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema katika sehemu nyingine ya hotuba yake kwamba sikukuu ya Nairuzi ni fursa nzuri ya kuweza kutekeleza maamrisho na hukumu za Kiislamu na kuongeza kuwa, wananchi wa Iran katika kipindi cha miaka mingi na hasa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu wamekuwa wakitumia sikukuu ya Nairuzi katika masuala ya umaanawi, maarifa na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na mfano wake wa wazi ni dua na tawasuli za mkusanyiko mkubwa wa watu wakati unapoingia mwaka mpya katika maeneo mbali mbali matakatifu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kwamba, taifa la Iran siku zote limekuwa likitumia suna hiyo kwa ajili ya kujiimarisha kidini, kimaanawi na kimaadili ya Kiislamu.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Ayatullah Waidh Tabasi, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala huko Kuharasan ambaye pia ni Mdhamini wa Haram ya Imam Riadha, ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa kuingia mwaka mpya wa Hijria Shamsia na amemkaribisha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano huo.
765923